……………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mnyama Simba ameunguruma mbele ya Mitutu ya JKT Tanzania na kutuma salama kwa watani zao Yanga baada ya kufanya mauaji ya kutisha ya mabao 4-0 dhidi ya wenyeji JKT Tanzania Mchezo uliomalizika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Wakicheza kwa Mpira wa Kibrazi Wekundu hao walianza kuonyesha makali dakika ya 3 bao likifungwa na Mshambuliaji hatari ukanda wa Afrika Mashariki Medie Kagere na Chris Mugalu aliwanyanyua tena mashabiki dk 6 akipachika la pili.
Kagere alirudi tena kambani dakika ya 40 kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa JKT hadi mapumziko Simba walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili Simba waliendelea kuuwasha moto dakika ya 54 winga hatari Luis Miquison aliiandikia bao la nne timu yake kwa shuti kali na kuufanya uwanja ulipuke kwa shangwe kutokana na uwanja kujaa mashabiki wakiwa na jezi Nyeupe na Nyekundu.
Kwa ushindi huo Simba wametuma salamu kwa watani zao Yanga ambao nao walishinda jana kwa mabao 3-0 wakimfunga Coastal Union huku Wakimtimua kocha wao.
Simba wanatarajia kukutana na Yanga mnamo Oktoba 18 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dodoma na kwa sasa Ligi itasimama kupisha Mchezo wa timu ya Taifa itakayocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Burubdi Oktoba 11 uwanja wa Mkapa.
Kwa Matokeo hayo Simba wamerudi kileleni mwa Ligi wakiwa na pointi 13 sawa na Yanga ila wakiwa na mabao mengi ya kushinda na Azam FC akishuka nafasi ya tatu wakiwa na Pointi 12 na wanamchezo Mmoja.
Matokeo mengine Biashara United imetumia vyema uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kwa kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0.
Mchezo wa mwisho kwa Leo utakuwa majira ya saa 1:00 usiku Azam FC watakuwa kwenye dimba lao la Chamazi wakiwakaribisha Kagera Sugar kutoka mjini Bukoba.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa Mechi moja kuchezwa uwanja wa Uhuru jijini Dar Es Salaam,wenyeji KMC watamenyana na timu ya Polisi Tanzania.