NA EMMANUEL MBATILO-0673956262
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 70,000 hufariki kila mwaka Duniani kutokana na Ugonjwa wa Kichaa Cha Mbwa.Kwa hapa nchini taarifa za tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa takribani watu 1,500 hufariki kila mwaka kwa ugonjwa huu.
Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa unasabibishwa na Virusi (Lyssavirus) vinavyoshambulia mfumo wa fahamu na ubongo.Ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya mnyama mwenye Kichaa cha Mbwa kumng’ata binadamu au wanyama wengine.
Kuna uwezekano wa kuambukizwa kichaa cha Mbwa baada ya kuumwa na Mbwa asiyeonyesha dalili za ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa. Hivyo kila tukio la kung’atwa na Mbwa ni lazima litolewe taarifa kwa mtaalamu wa afya au mifugo.Ungonjwa huu hauna tiba kwa binadamu au wanyama pindi dalili zinapojitokeza.
Mwaka huu, wamepatikana na watu 18,766 mfumo haujaripoti vifo,wengine wanahusisha na ushirikina kutokana na dalili zake kwahiyo wengine wanaenda kwa waganga wa kienyeji na wanafariki.
Wakati wa mahojiano na mtaalamu wa afya ya jamii kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto, Bi. Jubilate Bernard alisema wapo watu katika jamii wanahusisha dalili za ugonjwa huo na mambo ya kishirikina kitu ambacho sio sahihi.
“Mwaka huu, wamepatikana na watu 18,766 mfumo haujaripoti vifo,wengine wanahusisha na ushirikina kutokana na dalili zake kwahiyo wengine wanaenda kwa waganga wa kienyeji na wanafariki,”alieleza Bi.Jubilate.
DALILI ZA KICHAA CHA MBWA KWA WANYAMA
Dalili za kichaa cha mbwa hujitokeza kati ya siku mbili hadi siku 45 au zaidi tangu kung’atwa na mbwa au mnyama mwenye ugonjwa.Dalili hizo ni kama zifuatazo;
- Mbwa kubadilika tabia na kuwa mpole zaidi au mkali.
- Kushambulia na kuuma vitu mbalimbali kama vyuma,vijiti.
- Kushindwa kula na kunywa maji.
- kutokwa na mate mengi.
- kudhoofu,kupooza na hatimaye kifo.
Dalili hizi na nyinginezo zinaweza kujitokeza kwa wanyama wengine, kama vile mbuzi,ng’ombe,paka na nguruwe.Kichaa cha Mbwa huwapata wanyama pori pia, hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari pindi wanyama pori kama vile mbweha,fisi,mbwa mwitu na nguchiro wanapoonekana katika makazi ya watu.
UDHIBITI WA KICHAA CHA MBWA KWA WANYAMA
Chanja Mbwa na paka wako mara moja kwa mwaka au kulingana na ushauri wa mtaalamu wa mifugo.Ni muhimu kuzingatia hili kwa kuwa zaidi ya asilimia 95 ya maambukizi ya kichaa cha mbwa husababishwa na kung’atwa na mbwa mwenye ugonjwa.
Pia zingatia ufugaji bora wqa mbwa kwa kuhakikisha kuwa mbwa anapatiwa mahitaji muhimu na hazururi.Mbwa afungwe kuanzia saa 10:30 alfajiri hadi saa 4:00 usiku au kulingana na sheria ndogondogo za sehemu husika.
DALILI ZA KICHAA CHA MBWA KWA BINADAMU
Dalili za kichaa cha Mbwa kwa hujitokeza kati ya wiki moja hadi mwaka tangu kung’atwa na mbwa au mnyama mwenye kichaa cha mbwa.Dalili hizo ni kama zifuatazo;
- Kuchanganyikiwa
- Kuweweseka
- Homa
- Kuumwa Kichaa
- Maumivu ya Mwili
- Kuwashwa seheme ya jeraha
- Kuogopa kunywa maji
- Kudhoofu,kupooza kwa mwili na hatimaye kufa.
UDHIBITI WA KICHAA CHA MBWA KWA BINADAMU
Mtu aliyeng’atwa na mbwa au mnyama mwenye Kichaa cha Mbwa ni lazima apatiwe chanjo haraka iwezekanavyo kumuepusha kifo kutokana na ugonjwa huu.
Watoto waelimishwa kutokucheza au kuchokoza mbwa kwani asilimia kubwa watoto ndio wanaong’atwa na mbwa.
KUMHUDUMIA ALIYENG’ATWA NA MBWA AU MNYAMA
- Safisha jeraha kwa maji mengi na sabuni au tumia iodune au spirit
- Kidonda cha mtu aliyeng’atwa na mbwa au mnyama hakifungwi wala kushonwa .
- Kisha nenda kituo cha Afya kulicho karibu ili kupatiwa chanjo na matibabu zaidi.
- Vilevile toa taarifa kwa mtaalamu wa mifugo wa eneo husika.