Mgombea Ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM, Halima Okash akimnadi Mgombea Udiwani wa Kata ya Mpuyungu, Jimbo la Mvumi, Anthony Sakalani.
Okash akimuombea kura kwa unyenyekevu Mgombea Urais wa CCM. Dk. Magufuli, Mgombea Ubunge Jimbo la Mvumi, Livingstone Lusinde (Kibajaji) na Mgombea Udiwani, Sakalani.
Okash (wa pili kushoto) akimwaga sera za CCM katika kikao maalumu cha kampeni katika Kata ya Chinangali.
Na Mwandishi Wetu, Mvumi.
MGOMBEA Ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Halima Okash amewasihi wanawake waache kudanganyika bali wasimame imara kulinda kura zao kwa kumpigia mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli ambaye anawathamini.
Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni kwenye kampeni za CCM katika Kata ya Mpuyungu, Jimbo la Mvumi, ambapo alimnadi Mgombea Udiwani wa Kata hiyo, Anthony Sakalani, Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, Livingtone Lusinde na Mgombea Urais wa CCM, Dk. Magufuli.
“Nawasihi wanawake wenzangu msimame imara msije mkadanganyika, kura zenu ndiyo mkombozi wetu, tumpeni Dk. Magufuli ambaye ametuthamini mno hasa kwa uamuzi wake wa kumteua tena mwanamke mwenzetu, Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wake wa urais,”amesema Okash huku akishangiliwa.
Amesema kuwa, Dk. Magufuli amemteua tena Mama Samia ambaye ameonesha ujasiri wa uchapakazi katika miaka mitano akiwa Makamu wa Rais katika Serikali yake ya Awamu ya Tano. “Hakika Mama Samia ameonesha dhahiri kwamba wanawake tukipewa nafasi tunaweza,” amesema Okash.
Okash, mwanamke mpambanaji ambaye licha ya kuzisaka kura za wagombea wa CCM katika vikao vya ndani, mikutano ya kampeni, lakini vile vile amekuwa akizitafuta katika vijiwe vya kahawa, kwa Mama Lishe, sokoni, salon na vikundi mbalimbali vya akina mama.
Anapokwenda maeneo hayo, Okash amekuwa akitangaza sera za CCM, mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk Magufuli, lakini pia amekuwa akiwaeleza mazuri yaliyomo kwenye Ilani ya chama hicho yatakayoanza kutekelezwa mara baada ya CCM kupata ridhaa ya kupigiwa kura nyingi na wananchi.