Home Siasa UWT WILAYA DODOMA YASAKA KURA ZA USHINDI WAGOMBEA WA CCM

UWT WILAYA DODOMA YASAKA KURA ZA USHINDI WAGOMBEA WA CCM

0

Katibu wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Dodoma Mjini (UWT), Diana Madukwa akizungumza na wanawake wa Kata ya Makole alipofanya ziara ya kata kwa kata kuzungumza na wanawake wa Wilaya hiyo kwenye vikao vya ndani.

Katibu wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Dodoma Mjini (UWT), Diana Madukwa,akiwaonyesha na kuwahimiza  wanawake wa Kata ya Makole kutunza kadi ya kupigia Kura na kuepuka vishawishi vya kudanganya alipofanya ziara ya kata kwa kata kuzungumza na wanawake wa Wilaya hiyo kwenye vikao vya ndani.

Sehemu ya Wanawake wakimsikiliza Katibu wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Dodoma Mjini (UWT), Diana Madukwa (hayupo pichani) wakati akizungumza na wanawake wa Kata ya Makole alipofanya ziara ya kata kwa kata kuzungumza na wanawake wa Wilaya hiyo kwenye vikao vya ndani.

Mgombea udiwani kata ya Makole, Omary Haji,akiwaomba kura wanawake wa Kata ya Makole.

…………………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

Kamati Maalum za Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi(UWT), Wilaya ya Dodoma, zinazohusika na vikao vya ndani leo zimeendelea kwenye Kata ya Makole, Chamwino na Kizota, ambapo wameomba wananchi wa Dodoma kumchagua Rais John Magufuli na wagombea wote wa CCM kwa kuwa ndio watakaowaletea maendeleo ya kweli.

Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu wa UWT Wilaya hiyo, Diana Madukwa amewaomba kuwachagua wagombea hao ili kupata ushindi wa kishindo utakaowawezesha kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

“Mchague Anthony Mavunde kwa maendeleo ya jimbo la Dodoma mjini, lakini hakuna asiyemjua Rais John Magufuli ameipenda Dodoma na ulimwengu mzima unafahamu, ukitaja Dodoma unataja moyo wa Magufuli,”amesema.

Katibu huyo amesema Dodoma hakukuwa na soko la kisasa, kwasasa lipo na ni soko bora Afrika mashariki pia imejengwa stendi mpya ya mabasi na ndani ya miaka miwili imekamilika.

“Kituo cha afya Makole kilikuwa kidogo lakini umefanyika upanuzi ambapo sasa kuna jengo la akina mama la kujifungulia, Makole hakukuwa na barabara za lami sasa kwenye mitaa kuna barabara na taa zimeanza kuwekwa huyu si mwingine ni Magufuli,”amesema.

Ameeleza kuwa mwaka 1973 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema Makao Makuu yawe Dodoma lakini hayakuletwa kwa miaka 47, lakini baada ya kuingia madarakani Rais Magufuli yamehamia ndani ya mwaka mmoja.

Aidha, amewaasa wanawake kutokubali kutoa vitambulisho vyao vya kupigia kura kwa watu wanaopita kwenye maeneo yao wakiahidi kuwapatia mikopo.

“Kuna watu wameanza kupita wanachukua vitambulisho hivyo wakiahidi kuwapatia mikopo hawa wanachukua na kwenda kutoa ‘copy’ ambayo inakuwa ngumu kama kitambulisho, siku ya kwenda kupiga kura unakuta tayari ulishapiga kura kumbe hujapiga, ndugu zangu msikubali kuwapa watu hao wanaokusanya vitambulisho kitambulisho ni haki yako wewe kwa hiyo nawakumbusha mkatunze vitambulisho vyenu,”amesema.

Ameongeza “Ifikapo Oktoba 28 chukua kitambulisho vizuri ulipokitunza na ukapige kura kuchagua wagombea wa CCM ambao ndio watawaletea maendeleo ya kweli.”

Kwa upande wake, Mgombea udiwani kata ya Makole, Omary Haji amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kimsingi na kuchagua viongozi bora wa CCM.

“Tukampe heshima Rais wetu Magufuli kama alivyotupa heshima wanadodoma, tumpe heshima Mbunge wetu Mavunde ili afanye kazi aliyobakisha, na Mimi pia mnipe kura nyingi za kutosha niwatumikie wana Makole, nawaahidi tutakuwa bega kwa bega kuleta maendeleo kwa kata yetu,”amesema.