Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu na wenye ulemavu),Profesa palamagamba Kabudi, amevitaka vyama vya siasa nchini kutumia Baraza la Vyama vya Siasa kama jukwaa la mazungumzo katika kutatua tofauti na changamoto zinazojitokeza, akisisitiza kuwa hakuna jambo lisiloweza kumalizwa kwa mazungumzo.
Kabudi ameyasema hayo Octaba 7,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa akizindua uongozi mpya na nembo ya Baraza la Vyama vya Siasa, amesema mfumo wa vyama vingi haupaswi kutafsiriwa kuwa uadui, chuki, vitisho au uhasama, bali ni nafasi ya vyama vyenye mitazamo tofauti kukutana na kujadili mustakabali wa taifa.
Amesema viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kuheshimiana na kuvumiliana, kwa kuwa tofauti za kisiasa ni sehemu ya demokrasia na hazipaswi kuathiri amani, utulivu na umoja wa kitaifa uliopo nchini.
“Hakuna mwenyewe katika siasa. Mfumo wa vyama vingi ni kuwasaidia Watanzania wenye maoni na mawazo tofauti kukaa pamoja, kujadili na kuamua kuhusu mustakabali wa taifa lao,” alisema Kabudi.
Amesema Serikali ina jukumu la kuwezesha na kuratibu shughuli za vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria, huku akisisitiza kuwa masuala ya udhibiti yanaongozwa na Katiba na sheria, hivyo vyama vinapaswa kutumia fursa zilizopo kuwasilisha hoja na changamoto zao kupitia mifumo rasmi.
Kabudi amewataka viongozi wa vyama ambavyo vimekuwa vikisusia baadhi ya vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa kurejea na kushiriki, akisema baraza hilo ni jukwaa la pamoja linalopaswa kutumiwa na vyama vyote kujadili masuala yenye maslahi kwa taifa.
“Njooni tukae pamoja, sisi wote ni watoto wa nyumba moja. Hakuna jambo linaloshindikana katika mazungumzo,” amesema.
Aidha, amewataka wanasiasa kuzingatia matumizi ya lugha ya staha wanapotoa hoja au kukosoa wenzao, akisema demokrasia ya kweli inahitaji kuheshimu utu wa mtu na kutofautiana kwa hoja bila kutumia lugha za matusi, vitisho au zinazodhalilisha wengine.
Aidha Profesa Kabudi amesema Tanzania imejenga utamaduni wa kuvumiliana na kuishi kwa amani licha ya kuwepo kwa tofauti za kisiasa, kidini, kikabila na kijamii, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kulindwa na kuendelezwa na kizazi cha sasa.
Katika hatua nyingine, ameipongeza Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuzindua uongozi mpya pamoja na nembo yake, akisema hatua hiyo inaongeza utambulisho wa taasisi hiyo na kuimarisha nafasi yake katika kuratibu majadiliano na mashauriano miongoni mwa vyama vya siasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Alli khatibu, amesema chimbuko la baraza hilo ni mwafaka wa CCM na CUF wa mwaka 2001 uliolenga kurejesha amani, kuimarisha demokrasia na kujenga maridhiano ya kisiasa Zanzibar, kabla ya jukwaa hilo kupanuliwa na kuhusisha vyama vingine vya siasa.
Amesema kwa sasa baraza lina wajumbe kutoka vyama vya siasa vyenye usajili kamili na lina majukumu ya kutoa ushauri kuhusu migogoro ya kisiasa, masuala yenye maslahi ya taifa, sheria na kanuni zinazohusu vyama vya siasa, pamoja na kuhamasisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa.
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema ofisi yake itaendelea kuratibu na kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya baraza, huku akiwataka viongozi wapya kulinda utamaduni wa mazungumzo na ushirikiano miongoni mwa vyama vya siasa, akisema Tanzania imekuwa mfano wa nchi inayoweza kukaa pamoja na kujadili tofauti zake kwa amani.

