Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa Afrika na nchi za Nordic katika usimamizi wa Akili Unde (AI), huku akisisitiza umuhimu wa Afrika kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kimataifa kuhusu teknolojia hiyo.

Akizungumza Novemba 20, 2026, jijini Oslo, Norway, wakati wa Mkutano wa 23 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Nordic na Afrika, Mhe. Kombo amependekeza kuundwa kwa kamati ya pamoja yenye wajumbe 10, watano kutoka kila upande, itakayopendekeza hatua za kuendeleza matumizi salama na yenye manufaa ya AI.

Amesema pamoja na fursa za teknolojia hiyo katika kuchochea maendeleo, Afrika inapaswa kujiandaa kukabiliana na athari za matumizi mabaya ya AI. Aidha, amependekeza kuandaliwa kwa mkakati wa pamoja wa Afrika kuhusu AI ili kuimarisha uwezo wa bara hilo kunufaika na maendeleo ya teknolojia na kuhakikisha uwakilishi wake katika mifumo ya kimataifa ya usimamizi.

Naye, Mwenyekiti wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Espen Barth Eide, amesisitiza dhamira ya kuimarisha ushirikiano na Afrika katika sheria za kimataifa, biashara, uwekezaji na teknolojia mpya. “Tunataka kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika katika maeneo mbalimbali, kuanzia sheria za kimataifa hadi biashara, uwekezaji na teknolojia mpya.”

Mkutano huo, ulioshirikisha nchi 35 za Afrika na Nordic pamoja na Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia Siasa, Amani na Usalama, umejadili pia kuimarisha biashara, uwekezaji, upatikanaji wa mitaji nafuu, nishati safi, mabadiliko ya tabianchi na mageuzi ya taasisi za kimataifa.

Aidha, Ghana imechukua Uenyekiti wa Mkutano wa 24 wa Nordic – Africa wa mwaka 2027 utakaofanyika jijini Accra.