Afisa Uhusiano wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) tawi la Moshi, Neema Soka akimueleza jambo Mgeni rasmi katika maonesho ya siku ya Kahawa (Kahawa Festival) Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dk. Anna Mghwira alipotembelea banda la benki hiyo kufahamau namna ambavyo benki hiyo inasaidia sekta ya kilimo.
Afisa wa Huduma kwa wateja wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) tawi la Moshi, Rajab Mchomvu akitoa maelezo kwa mmoja wa watu waliotembelea banda hilo kwa lengo la kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.kushoto kwake ni Afisa Uhusiano wa Benki hiyo tawi la Moshi,Neema Soka.
Afisa uhusiano wa wateja binafsi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Kanda ya Kaskazini, Erick Mpopo akifafanua juu ya huduma za benki hiyo kwa Genes Mng’anya aliyefika katika Banda la NBC katika maonesho ya Kahawa Festival yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru Park mjini Moshi.
………………………………………………………………..
Ni kupitia maonesho ya Kitaifa ya Kahawa yanayofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Moshi. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeshiriki katika maonesho ya kwanza ya Kahawa nchini huku ikijikita katika kuwawezesha wakulima pamoja na wafanyabiashara wa zao la kahawa kuongeza thamani ya zao hilo ili liwe na tija zaidi katika uchumi wa Taifa.
Maonesho ya Kahawa kitaifa yanafanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo yatahusisha wadau mbalimbali kwa lengo la kusherekea siku ya Kahawa Duniani (International Coffee Day) ambayo hufanyika kila Oktoba mosi duniani ili kutambua mchango wa wadau mbalimbali kuanzia wakulima, waandaaji wasambazaji,na wauzaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonesho hayo, Meneja wa Benki hiyo Tawi la Moshi, Lazaro Mollel alisema benki hiyo imejizatiti katika kuhakikisha zao la Kahawa linachangia katika ukuzaji wa uchumi wa Taifa kupitia hasa katika kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara kuongeza ufanisi kwenye mazao yao.
“Tunafarijika kuwa sehemu ya maonesho haya makubwa ya Kahawa, kama benki ya biashara tumejizatiti kuhakikisha kwamba zao la Kahawa linakuwa na tija katika ukuaji wa uchumi kwa kufanya jitihada mbalimbali ikiwamo kutoa mikopo kwa wakulima pamoja na kutoa mafunzo ya namna bora ya kuendeleza kilimo biashara,” alisema Mollel.
Zao la Kahawa ni kati ya mazao makuu ya biashara yanayouzwa kwenye soko la kimataifa likikadiriwa kufikia asailimia 5 ya mazao yote yanayouzwa kwenye soko hilo.Pia, asilimia 90 ya zao la kahawa linatoka kwa wakulima wadogo.
Naye, Meneja Mahusiano wa NBC, Neema Soka alisema Katika kuhakikisha wakulima wanapata huduma za kibenki kwa uhakika na haraka zaidi, Benki ya NBC inatoa huduma ya akaunti ya NBC Shambani na NBC Kiganjani ambazo zinamsaidia mkulima kuhifadhi na kuzifikia fedha zakwa wakati wowote.
“Huduma ya NBC Shambani inawalenga wadau wote wa kilimo wakiwamo wasambazaji, wakulima, wauzaji wa pembejeo na pia inatoa fursa kwa wakulima wanaofanya kazi kwenye vikundi vya ushirika (Amcos) kufungua akaunti ya kikundi kufungua akaunti ya pamoja na ya mtu mmoja mmoja ambazo uendeshaji wake ni bure,” alisema.
Mbali na kutoa huduma za kibenki kama kufungua akaunti mpya, benki hiyo hutoa mafunzo kwa wajasiriamali kupitia program ya NBC Kliniki kuhusu masuala ya usimamizi wa fedha na biashara ili kuwawezesha kukuza biashara zao.