…………………………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Songea
MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Pololet Kamando Mgema,ametao saa 24 kwa Halmashauri ya wilaya ya Songea kukamilisha ujenzi wa jengo la Mama na mtoto katika Hospitali ya wilaya ili liweze kutoa huduma kwa akina mama ambao hadi sasa wanateseka kwa kwenda hadi hospitali ya rufaa Songea na hospitali ya misheni Peramiho kufuata huduma za matibabu.
Mgema ametoa agizo hilo leo(jana) baada ya kufanya ziara ya kustukiza kukagua ujenzi wa Hospitali hiyo inayojengwa katika kijiji cha Mpitimbi ambapo alikuta agizo lake la siku 7 kwa halmashauri kukamilisha jengo hilo na majengo mengine halijatekelezwa licha ya serikali kutao fedha zote za ujenzi.
Ujenzi wa hospitali ya wilaya Songea ulianza mwaka 2019 na ulitakiwa kukamilika mapema 2020 ambapo katika awamu ya kwanza serikali ilitoa shilingi bilioni 1.5 na awamu ya pili iliongeza milioni 300 ili kukamilisha kazi na unajengwa kwa mfumo wa force account.
Hata hivyo,kutokana na usimamizi mbovu baadhi ya majengo bado hayajakamilika ambapo hadi sasa jengo lililoanza kutoa huduma ni moja la wagonjwa wa nje(OPD) jambo lililomfanya mkuu wa wilaya kutoa siku mbili kwa halmashauri kuhakikisha wanakamilisha majengo yaliyobaki.
“wiki iliyopita nilikuja hapa kuangalia ujenzi unavyoendelea,lakini sikuridhishwa na kasi ya mafundi, nikatoa wiki mmoja kwa halmashauri kukamilisha kazi zilizobaki, hata hivyo jambo la kusikitisha maeneo ambayo niliyaacha yakiwa na mapungufu leo nimeyakuta yako vile vile”alisema Mgema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema, vifaa vyote kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo hayo vipo lakini tatizo liko kwa wasimamizi wa mradi huo,hivyo kuchelewesha wananchi kupata huduma.
Kwa mujibu wake,kazi ambazo hadi sasa hazijakamilika ili hospitali hiyo ianze kufanya kazi ni mfumo wa maji safi na maji taka,kufunika mashimo ya choo,kurekebisha milango na kupeleka umeme kazi ambazo kama halmashauri wangekuwa makini na uchungu kwa wananchi zilipaswa kukamilika tangu mwezi juni mwaka huu.
“mkuu wa mkoa alifika hapa na aliagiza umeme ufike,lakini nasikitika kuona hata agizo la mkuu wetu wa mkoa halijatekelezwa, katika halmashauri hii ya Songea shida tupu, sijui hawa watendaji wana muhujumu mkurugenzi wao ili afukuzwe kazi mimi nashindwa kuelewa”alisema mkuu wa wilaya.
Kwa upande wake afisa mipango wa halmashauri ya Songea vijijini Nyanga Athuman ambaye alikutwa katika eneo hilo alikiri kuchelewa kwa ujenzi wa hospitali hiyo, hata hivyo alijitetea kwamba tatizo ni mafundi waliopewa kazi.
Alisema,agizo la mkuu wa wilaya watalifanyia kazi haraka kwani kazi zilizobaki ni kidogo ikilinganisha na zilizofanyika.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mpitimbi B ambaye ni mumbe wa kamati ya ujenzi wa Hospitali Salum Msanga alisema, wananchi wanaendelea kupata changamoto ya matibabu kwa kutembea hadi Hospitali ya misheni Peramiho na hospitali ya rufaa mjini songea kufuata matibabu.
Alisema, kama ujenzi huo utakamilika haraka itakuwa faraja kubwa kwa wananchi wa kijiji hicho na kata yote ya Mpitimbi kwani itasaidia kusogeza huduma na hivyo kuokoa muda wa kufuata matibabu mbali na muda huo watautumia kufanya shughuli nyingine za kujiletea maendeleo.