Mkurugenzi wa udhibiti ubora Shirika la viwango Tanzania TBS Bw.Lazaro Msasalaga akizungumza wakati akitoa mafunzo kwenye semina kwa wazalishaji,wasambazaji,na wauzaji wa mafuta ya kula yaliyofanyika leo jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo wakimsikiliza Mkurugenzi wa udhibiti ubora Shirika la viwango Tanzania TBS Bw.Lazaro Msasalaga (hayupo pichani) akitoa mafunzo kwenye semina kwa wazalishaji,wasambazaji,na wauzaji wa mafuta ya kula yaliyofanyika leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa udhibiti ubora Shirika la viwango Tanzania TBS Bw.Lazaro Msasalaga akizungumza na waandishi wa habari mara baada kutoa semina kwa wazalishaji,wasambazaji,na wauzaji wa mafuta ya kula yaliyofanyika leo jijini Dodoma.
Mzalishaji mdogo wa mafuta ya alizeti,Daudi Makala,akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafunzo walivyopata faida kutokana na semina kutoka TBS kwa wazalishaji,wasambazaji,na wauzaji wa mafuta ya kula yaliyofanyika leo jijini Dodoma.
Muuzaji kutoka soko la saba saba Bi.Eunice Maneno,akielezea elimu waliyoipata kutoka na semina kutoka TBS kwa wazalishaji,wasambazaji,na wauzaji wa mafuta ya kula yaliyofanyika leo jijini Dodoma.
……………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
SERIKALI imesema ipo kwenye mchakato wa kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini kwa mazao yote yanayotoa mafuta ikiwemo alizeti, na michikichi ili kupunguza gharama za kuingiza mafuta kutoka nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa udhibiti ubora {TBS} Bw.Lazaro Msasalaga wakati akitoa mafunzo kwenye semina kwa wazalishaji,wasambazaji,na wauzaji wa mafuta ya kula.
Mafunzo haya yamelenga kuwaelimisha wadau hao juu ya uzalishaji bora, uhifadhi sahihi wa bidhaa za mafuta haswa sehemu za kuuzia, ufungashaji sahihi na salama na umuhimu wa kuzingatia na kuweka taarifa sahihi na muhimu katika vifungashio.
Amesema lengo kubwa la serikali ni kuzingatia mahitaji makubwa ambayo kwa sasa wananchi wanahitaji ili kuweza kuzalisha mafuta ya kula kwa wingi nchini.
“Waziri ana mradi mkubwa wa kupanda michikichi kule Kigoma lengo kubwa ni kuongeza uzalishaji wa mafuta nchini, na si kwenye michikichi tu inaenda kuangalia na uzalishaji wa mazao mengine kama alizeti na namna Mkoa husika unavyoweza kuzalisha zao hilo“ amesema Msasalaga
Aidha amesema katika mafunzo hayo wamepita wilaya zote za mkoa wa Dodoma, Singida na Tabora ili kuweza kuwaelimisha wazalishaji na wauzaji namna ya kuyatunza mafuta ili yawe na ubora.
“ Tumeenda Kongwa Kibaigwa,Mpwapwa, Chamwino, Kondoa, na wengine wapo mikoa ya Singida na Tabora, tukitoka Dodoma jiji tutamalizia Bahi, Manyoni na Itigi kuendelea kusambaza elimu hii japo Kuna changamoto ambazo tunazipata lakini nasi tunaziwekea mikakati kiukweli kama mafuta yasipofungashwa vizuri kwa kupigwa na mwanga wa jua mafuta yanaweza kuharibika”
Amesema katika mafunzo hayo wanasisitiza katika uhifadhi ndio maana wamewatembelea wauzaji wa barabarani waweke vibanda kukinga mafuta kwani jua linapopiga mafuta yanaharibika.
Msasalaga ametoa ushauri kwa wadau hao kuzingatia kanuni za uzalishaji na uhifadhi bora na salama ili kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu ambayo itawalazimu kuteketeza kwa gharama zao.
Naye Daudi Makala, Mzalishaji mdogo wa mafuta ya alizeti amesema kuwa wamejifunza namna ya kuzingatia ubora wa mafuta kwani kwa kufanya hivyo atampa uhakika mtumiaji .
“ Pia tuhakikishe mbegu imekomaa na usafi pamoja na utayalishaji wa mafuta haya kiukweli tumejifunza mambo mengi tukizingatia nafikiri walaji watafurahia ,sisi wasindikaji wa mafuta inabidi sasa mara kwa mara tuwe na semina ili tuweze kukumbushana “ amesema Makala
Muuzaji kutoka soko la saba saba Bi.Eunice Maneno amesema kuwa kutokana na semina amejifunza mambo mengi kutoka kwa mkulima hadi kufikia mafuta yenyewe .
“ Wakati mwingine unaweza kununua mafuta machungu kumbe ni kutokana na mkulima kukimbilia soko anaweza akakamua mafuta ambayo mbegu haijakauka kwahyo mi niombe tu semina hizi tuzipate mara kwa mara na niwaombe wananchi watumie mafuta haya ya alizeti kwani ni mazuri kwa afya”.Amesema Eunice.
Mpaka sasa wadau zaidi ya 400 kutoka Kongwa, Chamwino, Mpwapwa, Kibaigwa,Kondoa na Dodoma Mjini wamefikiwa na mafunzo haya, ambapo maeneo ya Bahi watafikiwa kesho tarehe 29.09.2020.