Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Bukoba Vijijini, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Rubale, Kata ya Rubale, Jimbo la Bukoba Vijnijnini,
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwakabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Rubale, Kata ya Rubale, Jimbo la Bukoba Vijnijnini, Septemba 28, 2020. Katikati ni Diwani wa Kata ya Rubale, Renatus Rwegasira(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………….
MJUMBE wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ya CCM imedhamiria kuhakikisha kilimo kinamnufaisha mkulima wa Tanzania.
“Watu wasije kuwadanganya kwamba Serikali haiwajali, siyo kweli. Kuna sababu zilizochangia kuyumba kwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia.”
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Septemba 28, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Rubale kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Rubale, wilayani Bukoba, mkoani Kagera.
“Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, iliazimia kufufua mazao matano ya kimkakati ambayo ni kahawa, pamba, korosho, chai na tumbaku. Mazao haya bei ilishuka na si katika zao la kahawa tu.”
“Kuyumba kwa bei haikuwa katika zao la kahawa tu bali katika mazao mengine kama pamba na korosho. Kahawa bei yake iliathirika kwa sababu ya ugonjwa wa Corona. Korosho bei ilishuka kutoka sh.3,300 hadi sh. 1,900. Pamba pia ilishuka bei,” amesema.
Amesema Kenya ndiko mnada wa kahawa huwa unafanyika lakini hadi sasa bado wanasumbuliwa na ugonjwa wa Corona kwa hiyo haikuwa rahisi kufanya biashara katika kipindi chote hicho.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye ameanza ziara katika mkoa wa Kagera kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli. Ametumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Bw. Jason Rweikiza, mgombea udiwani wa kata ya Rubale, Bw. Rwegasira Renatus Rwechungura na madiwani wengine wa jimbo hilo.
Kuhusu maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 4.09 zilitolewa ili kuboresha miradi ya maji katika vijiji kadhaa ambayo yote imekamilika. Almevitaja vijiji hivyo kuwa ni Ibwera, Kasharu, Kitahya, Katale, Itongo, Bituntu, Kibona, Katoro, Mikoni, Kibirizi Ngarama, Ruhoko na Ruhunga.