Mkuu wa Wilaya ya Magu,Salum Kalli (kushoto) akipanda mlima wa Kijiji cha Ijinga kisiwani kukagua tenki la mradi wa maji safi salama kwa ajili ya wananchi wa kisiwa hicho.
………………………………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, MAGU
WANANCHI wa Kisiwa cha Ijinga katika Wilaya ya Magu, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu maji safi na salama,umeme,daraja la kivuko na wanyama waharibifu wa mazao.
Walitoa kilio hicho kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Salum Kalli, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika maeneo ya Shule ya Msingi Ijinga jana.
Walisema licha ya kisiwa hicho kuzungukwa na maji hawana maji safi na salama ya bomba,umeme na daraja kwa ajili ya kivuko baada ya lililokuwepo kujengwa chini ya kiwango na kumezwa na maji.
“Umekuwa mkuu wa wilaya wa pili kuja kututembelea hapa kisiwani tangu mwaka 1961 , tunashukuru sana.Tuna changamoto ya umeme na maji, pia kero ya viboko (wanyama) wamekuwa wengi na wanaharibu mazao yetu,” alisema John Damas Buhomo.
Pia wanafunzi wa Shule ya Msingi Ijinga wakiongozwa na kiranja mkuu, waliomba kuongezewa walimu sita ili kupunguza uhaba wa walimu shuleni hapo huku Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ncheyeki Julius akiainisha changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu na uchakavu wa madarasa.
Alisema paa la vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu wa shule hiyo linahitaji kuboreshwa kutokana uchakavu una hatarisha maisha ya wanafunzi na walimu, ina upungufu wa madarasa 7 kati ya 15 (mabovu ni 4), walimu waliopo 8 kati ya 15 ambapo wawili wako masomoni,anahitajika mmoja wa kike, nyumba za walimu zinahitajika 10, zipo tano , mbili ni mbovu (hazifai).
Ncheyeki alisema shule hiyo ina wanafunzi 688 wasichana 341 na wavulana 347, madawati 120 kati ya 200, matundu 20 kati ya 32 na hivyo ili kutolesha idadi ya wanafunzi na kuiomba serikali iwasaidie kutatua changamoto hizo.
Akizungumzia suala la nishati ya umeme Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli, alisema wataalamu wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) watafika kisiwani hapo ili kuanisha njia ya kupitisha miundombinu ya nishati hiyo baada ya uchaguzi.
Kuhusu uhaba wa walimu alisema atawasiliana na Afisa Elimu ili walimu watakaopata ajira baadhi wapelekwe kisiwani hapo na kuahidi kuzungumza na mkuu wa idara ya maji kuona namna ya kuboresha,haiwezekani wananchi wa Kisiwa cha Ijinga wakose maji ilhali yamewazunguka.
Kalli alisema wazazi kisiwani humo watoe fursa kwa watoto wasome na kutimiza ndoto zao ili baada ya kuelimika watumie elimu na ubunifu wao kuwasaidia kutengeneza utalii wa aina yake huku akiwataka wananchi wa kisiwa hicho kuwalinda wazee dhidi ya mauaji ya kikatili yanayotokana na imani potofu za kishirikina ili waishi kwa amani.
“Shule hii imejengwa na serikali ya CCM na watoto wanasoma bure, kazi yenu wazazi hakikisheni mnawapa mahitaji yao ya kibinadamu watoto wasome bure wala msiwakubalie vijana wa ovyo ovyo waharibu maisha yao na watakaobainika wachukuliwe hatua,”alisema.
Akimuombea kura mgombea urais wa CCM Rais John Magufuli, Kalli alisema wasimsahau mgombea huyo ambaye amehangaika na shida za wanyonge badala yake wape kura nyingi ili akamilishe miradi ya maendeleo anayoijenga ikiwemo ya maji, barabara , hospitali, vituo vya afya na umeme.
Alisema ni muhimu wananchi wakachagua kiongozi atakayeleta amani, maendeleo, mpenda mabadiliko, mpenda Watanzania wanyonge na anayeweza kufanya hayo ni rais Dk. Magufuli.