………………………………………………………..
Na John Walter- Manyara
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally ametoa onyo kali kwa wale wote wanaopita kukusanya shadada za kupigia kura kwa visingizio vya kutoa mikopo kwa wananchi.
Ametoa onyo hilo Septemba 27, 2020 akiwa kata ya Engusero wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara akiwa ameongozana na Mgombea Mwenza wa CCM wa Urais Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan baada ya uzinduzi wa Kampeni awamu ya tatu kati ya sita, uliofanyika wilayani Kongwa mkoa wa Dodoma.
“Tusilaghaiwe, shahada yetu ya kupiga kura, ina kazi ya kupiga kura tusidanganywe kwamba shahada hiyo unaweza ukapata mikopo, ukiona mtu anakwambia hivyo mtafute mwenyekiti wa Kitongoji akamatwe na achukuliwe hatua za sheria.”
Katibu Mkuu ameongeza kuwa, “Ukiona mtu anakuhamasisha kufanya fujo, usimkubalie kwasababu nchi hii ni nchi huru na ni kisiwa cha amani.”
Awali, katika uzinduzi huo, Wilayani Kongwa Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kuzipongeza kamati za siasa za ngazi zote pamoja na wenyeviti wa mashina kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kuhakikisha ushindi mkubwa unapatikana.
Uzinduzi huo ni wa awamu ya tatu kati ya sita ambapo awamu ya nne itafanyika Zanzibar.