************************************
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kupeleka umeme kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza.
Hayo yalisemwa jana (Ijumaa, Septemba 25, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa, Kassim Majaliwa katika mkutano wa kampeni katika kitongoji cha Gana. Katika mkutano huo, Mheshimiwa Majaliwa alimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea mbunge, Bw. Joseph Mkundi na madiwani wa wilaya hiyo.
Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ijayo kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025, itaboresha huduma ya umeme katika visiwa vyote nchini kikiwemo Gana chenye wakazi zaidi ya 3000. “Mkakati wetu ni kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata umeme, Ukerewe vijiji 70 tayari vina umeme vimebaki sita ambavyo vitapitiwa na mradi,” alisema Majaliwa.
Alisema asilimia 80 ya vijiji nchini vimepata umeme baada ya Serikali ya awamu ya tano kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020. “Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuendeleza na kuimarisha sekta ya nishati ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali. Mpango wa Serikali ni kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote na maeneo ya pembezoni mwa miji.”
Majaliwa alisema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imepata mafanikio kwa kuzalisha umeme kutoka megawati 1,308 mwaka 2015 hadi 1,602 mwaka 2020 ongezeko ambalo limeifanya nchi kujitosheleza kwa mahitaji ya umeme.
Upatikanaji wa umeme kwa jumla Tanzania Bara umeongezeka kutoka asilimia 36 mwaka 2015 hadi asilimia 70. Ujenzi wa miradi umepunguza gharama za kuunganisha umeme vijijini kutoka wastani wa sh. 454,000 hadi 27,000.
Kuhusu sekta ya uvuvi, alisema Serikali imeondoa kodi katika bidhaa mbalimbali za uvuvi ili kutoa fursa kwa wavuvi kujipatia kipato na kuinua uchumi wa Taifa. Tayari Serikali imeondoa kodi katika zana na malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio.
“Tumedhamiria kuboresha sekta ya uvuvi kwa kuchukua hatua mbalimbali, tumeondoa kodi katika baadhi ya maeneo ili kuhakikisha wavuvi wanapata manufaa kutokana na kazi yao,” alisema Majaliwa.
Alisema Chama kupitia Ilani ya CCM, kitaimarisha ulinzi katika Ziwa Victoria kwa kununua boti za ulinzi ambazo zitawalinda wavuni wanapokuwa katika shughuli zao za uvuvi. Katika kuhakikisha wavuvi wanafanya kazi kwa ufanisi, Serikali iliimarisha ulinzi kwa kuanzisha Kanda Kuu tatu katika ukanda wa Ziwa Victoria, Tanganyika na Pwani. Pia zimeanzishwa kanda nne ndogo za Ukerewe, Sengerema, Nyumba ya Mungu na Mtera.