***************************************
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Hanang Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, mhandisi Samwel Hhayuma amesema akichaguliwa kushika nafasi hiyo atahakikisha anafanikisha uchumi wa viwanda kwa jamii kupitia rasilimali zilizopo eneo hilo.
Hhayuma aliyasema hayo jana kwenye kampeni ya kujinadi na kuomba kura kwenye kata ya Ganana, lengo likiwa ni kunyanyua uchumi wa wananchi wa Hanang’.
Alisema kupitia mazao ya ngano, mahindi na alizeti, viwanda vya nafaka vitaanzishwa ili kuongeza thamani mazao hayo tofauti na kuyauza yakiwa ghafi kwani yanauzwa kwa bei ndogo.
“Ardhi ya Hanang’ ina rutuba nzuri hivyo tunataka kupitia mazao hayo watu wanunue unga siyo mahindi, wanunue unga wa ngano, kuliko ilivyo hivi sasa ili kuongeza thamani mazao yetu na jamii kunyanyuka kiuchumi,” alisema Hhayuma.
Alisema kwenye kata ya Gendabi kuna madini ya chumvi napo kunapaswa kuwekwa kiwanda cha chumvi ili watu wakinunua chumvi iwe imefungwa kitaalamu na siyo kuwekwa kienyeji.
Alisema kwenye kata ya Mogitu kuna mawe yanayotengenezea saruji hivyo watahakikisha kiwanda kinajengwa ili wananchi wanunue saruji iliyozalishwa Hanang’ na siyo sehemu nyingine.
“Pia tunapaswa kuweka kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo ikiwemo nyama na ngozi ili kwa namna moja au nyingine tunyanyue uchumi wa wafugaji wetu wa Hanang,” alisema Hhayuma.
Mbunge mteule wa UVCCM Taifa, kutoka mkoani Manyara, Asia Halamga alisema wananchi wa Ganana walifanya makosa kipindi kilichopita hivyo wasirudie kwenye uchaguzi huu.
“Mlimchagua diwani ambaye kazi yake ilikuwa kupinga maendeleo hivyo tufanye uamuzi sahihi kwa kumchagua Isaya Mbise ambaye ataenda kuwatetea kwenye halmashauri ya wilaya,” alisema Halamga.
Mwenyekiti wa CCM wilayani Hanang’ Mathew Darema aliwataka wananchi wa eneo hilo wasikubali kuchezea kamari maisha yao kwa kutofanya uamuzi sahihi wakati wa uchaguzi.
Darema alisema CCM imewaleta wagombea sahihi kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani wenye sera hivyo wananchi wachague viongozi bora wa chama hicho.
Mgombea udiwani wa kata ya Ganana kwa tiketi ya CCM, Isaya Mbise alisema uchaguzi ni hatima ya maisha ya jamii kwa miaka mitano hivyo wasifanye makosa pindi wakichagua viongozi.
Mbise alisema akiwa mgombea udiwani yeye ni kijana mwenye uwezo wa kutumwa na wananchi na kisha akawatumikia kupitia nafasi hiyo.