********************************
Na Eleuteri Mangi, WHUSM-Dodoma
Tanzania ni kitovu cha lugha sanifu na fasaha ya Kiswahili Afrika Mashariki na duniani. Hayati Shaaban Robert ni miongoni mwa Watanzania wenye ubobevu katika lugha hiyo ambaye anathibitisha uhalisia huo kwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wanaokumbukwa kwa kuitendea haki lugha ya Kiswahili kupitia kazi zao.
Utaalam, ustadi na ujuzi wa Shaaban Robert katika lugha ya Kiswahili umempa sifa ya kuwa miongoni mwa wanazuoni wa mwanzo kuitupia jicho la kina dhana ya tafsiri kama taaluma na ni miongoni mwa waandishi wa kwanza wa utanzu wa Riwaya ya Kiswahili.
Wapenzi wa lugha ya Kiswahili humkumbuka Shaaban Robert kutokana na mchango na umahiri wake kwa kujikita katika kuandika vitabu vya riwaya na ushairi ambavyo vimekuwa kioo kwa jamii inayopenda lugha hii na kuitumia.
Kutokana na uandishi wake mahiri wa lugha ya Kiswahili na wenye kusadifu mazingira ya nchi yetu, mamlaka zinazohusika na ukuzaji mitaala ya elimu nchini ziliamua kutumia vitabu vyake katika kueneza na kujifunza fasihi ya Kiswahili ambapo baadhi ya vitabu vyake vimetumika na vinaendelea kutumika katika shule za sekondari na vyuo vikuu vya elimu ya juu. Baadhi ya vitabu vyake vilivyotumika na vinavyoendelea kutumika ni ‘Mapenzi Bora’, ‘Kufikirika’ ‘Kusadikika’, ‘Adili na Nduguze’, ‘Maisha yangu na baada ya miaka Hamsini’, ‘Barua za Shaaban Robert’, ‘Utu Bora ni Kilimo’ na ‘Wasifu wa Siti binti Saad.’
Wahenga walinena “Yakale ni dhahabu”, utaalamu wake katika lugha ya Kiswahili umekuwa msingi wa sifa kedekede anazopewa ambazo zinaambatana na kazi yake ya kukuza, kueneza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ambapo hakuna anaweza kubeza kazi yake ya kuandika vitabu vingi vya Kiswahili enzi za uhai wake. Shaaban Robert ameandika zaidi ya vitabu 20 ambapo vitabu vyote vina kila aina ya ufundi na vionjo mbalimbali vya lugha na hivyo kumfanya mtunzi huyu aitwe gwiji, galacha na bingwa wa lugha ya Kiswahili.
Vitabu vingene vya Kiswahili alivyoandika ni pamoja na Utu Bora, Almasi za Afrika, Mwafrika Aimba, Koja la Lugha, Insha na Mashairi, Ashiki Kitabu Hiki, Pambo la Lugha, Kielezo cha Fasili, Masomo Yenye Adili, Utenzi wa Vita vya Uhuru, Mashairi ya Shaaban Robert, Sanaa ya Ushairi, Siku ya Watenzi Wote, Kielelezo cha Insha, Mithali na Mifano ya Kiswahili.
Kufuatia kifo chake, Sheikh Amri Abedi aliandika ushairi uliojaa hekima na busara kuhusu umuhimu wa bingwa huyu wa lugha ya Kiswahili;
“Hae! Msiba mzito amefishwa Shaaban; Nyoyo zinawaka moto imetujaa huzuni; Lugha kwetu bado toto mlezi sasa ni nani? Kafariki Shaaban mlezi wa Kiswahili. Kwa kulea Kiswahili shekhe wetu Shaaban, Safu yake ya awali kwa tungo zenye thamani; Mahiri mwenye akili kwa tenzi hana kifani; Ole kafa Shaaban mlezi wa Kiswahili. Atokezapo kuranda kwa nui za ushindani, Hazuki wa kumshinda kwa rai zenye uzani; Kila hoja huipanda akatawala medani; Hae! Kafa Shaaban mlezi wa Kiswahili.”
Ushairi huo unaonesha Shaaban Robert alikuwa mtu wa namna gani katika kukuza, kueneza na kuendeleza lugha ya Kiswahili nchini kwani ni mtunzi ambaye kazi zake zinaendelea kulipatia heshima Taifa la Tanzania zikipambwa kwa ujumbe mzito uliomo katika mashairi na vitabu hivyo.
Fikra zake, tamaduni na uhusishaji wa lugha ya Kiswahili, utunzi na mantiki vimekuwa ndiyo vionjo vinavyomtofautisha Shaaban Robert na watunzi wengine wa vitabu vya riwaya na mashairi ya Kiswahili.
Ama kweli, ‘Chanda chema huvikwa pete’, hii ni methali ya Kiswahili inayosadifu kazi na uhodari wa hayati Shaaban Robert katika lugha ya Kiswahili. Uhodari huu ulimfanya apate tuzo ya “Margaret Wrong Memorial” kwa kazi iliyotukuka ya uandishi wa vitabu na mashairi kwa kutumia kipaji cha ushairi kwa kuthamini kazi na Taifa lake.
Aidha, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivutiwa sana na umahiri wa kazi za ushairi zilizotukuka za Shaaban Robert. Ni dhahiri baadhi ya Wanazuoni wa lugha ya Kiswahili wanadiriki kusema tangu Shaaban Robert afariki Juni 20, 1962 hakujatokea mtu aliyejipambanua kwa kuithamini na kuitukuza lugha ya Kiswahili kama alivyofanya Shaaban Robert enzi za uhai wake.
Kila mara ujumbe alioandika katika kazi zake alisisitiza kuheshimu kazi, utu bora na utiifu ambavyo ndiyo shabaha ya tunu za Taifa zinazolenga kuwa na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji na kuwa na Taifa lenye utamaduni unaojipambanua miongoni mwa mataifa mengine.
Hatua hiyo inaenziwa na Serikali ambapo imeifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Taifa ambapo pia inatumika katika kufundishia katika shule za msingi na kuwa somo katika shule za Sekondari na vyuo vya kati na vya juu. Hatua hizi zinaifanya lugha hii kuendelea kukua na kupanua wigo wa matumizi yake. Hivi karibuni Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imekuwa miongoni mwa watumiaji wa Kiswahili ambapo kiliingia kuwa lugha rasmi Agosti 18, 2019 baada ya kuridhiwa katika mkutano wa Wakuu wa nchi wanachama uliofanyika jijini Dar es salaam. Hatua hiyo inatoa fursa ya kuimarika kwa utalii wa kiutamaduni ikizingatiwa watu wa mataifa mbalimbali wanapenda kuja nchini kujifunza na kuifahamu zaidi lugha hii adhimu.
Profesa Mshiriki na Mgoda, Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere katika Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Aldin Mutembei amethibitisha kupanuka kwa lugha ya Kiswahili duniani katika makala yake “ Kiswahili kama lugha ya Mawasiliano mapana barani Afrika”, aliyoiwasilisha katika mkutano wa lugha za Afrika ,UNESCO uliofanyika jijini Paris Ufaransa mapema Februari 21 mwaka huu ambapo alisema kuwa Kiswahili ni lugha ya 10 kutumiwa duniani, na katika nchi za Afrika inatumiwa na watu milioni 224.9.
Aidha, lugha hii imepata umaarufu mkubwa duniani na inaendelea kukua hadi sasa kwa ajili ya mchango mkubwa wa Baba wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hoja ambayo ilitolewa Oktoba 14, 2013 wakati wa hafla maalumu ya kumuenzi mpigania uhuru huyo kwa mara ya kwanza kwenye Umoja wa mataifa.
Shime Watanzania, wanazuoni na taasisi zinazofundisha Kiswahili nchini, sasa ni muda mujarabu wa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kama alivyofanya Shaaban Robert ili lugha hii aushi na adhimu iendelee kuwa tunu na lugha ya Taifa.
Hakika usimamizi wa matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu katika utoaji wa huduma kwa wananchi yatalihakikishia taifa maendeleo na matumizi sahihi ya lugha hii ambayo yanaendelea kuimarisha na kuongeza wigo Afrika Mashariki, Afrika na duniani kote.