Mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Emmanuel Ole Landey (katikati) akishangilia na viongozi wa chama hicho kwenye uzinduzi wa kampeni ya chama hicho Mji mdogo wa Mirerani.
Wafurukutwa wa Chadema wa Mji mdogo wa Mirerani wakinyoosha mikono juu kumshangilia mgombea ubunge wa chama hicho wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Emmanuel Ole Landey akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya chama hicho.
………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya Chadema Emmanuel Ole Landey amewataka wapiga kuwa wa Simanjiro kutowachagua wagombea ambao walipata madaraka lakini wakashindwa kusaidia maendeleo hata jamii ya kwao.
Amesema wananchi wanapaswa kuepuka kudanganywa na wanasiasa wanaowaahidi kuwaletea maendeleo ili hali wameshindwa kufanikisha hayo kwenye maeneo waliyozaliwa.
Mgombea ubunge wa jimbo la Simanjiro mkoani Manyara, Emmanuel Ole Landey kwa tiketi ya Chadema, ameyasema hayo mji mdogo wa Mirerani, kwenye uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi ya chama hicho.
Ole Landey amesema kiongozi ambaye anawaeleza wananchi kuwa atawaletea maji wakati kijijini kwao alipozaliwa ameshindwa kufanikisha hilo kwani hakuna hata kisima cha maji huyo ni muongo.
Amesema mgombea atakayeahidi kuwajengea shule wakati alishindwa kujenga kijijini kwao na watoto wanatembea kilomita 30 kufuata shule eneo lingine huyo ni muongo.
Amesema endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo vipaumbele vyake vitakuwa elimu, afya, maji na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
“Mtu ameshakuwa mbunge kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita hajafanya chochote leo anakuja tena amesahau nini kama siyo tamaa za kimwili na tutazishughulikia,” amesema Landey.
Aliyekuwa mjumbe wa baraza kuu la Chadema, Joseph Kasambala amesema chama hicho kikiingia madarakani watawarudisha kazini wafanyakazi waliofukuzwa kwa ajili ya vyeti kwani hawakujiajiri.
Kasambala amesema hivi sasa wananchi mitaani hawana fedha hadi baadhi ya wanaume wanaondoka majumbani mwao asubuhi kwa kujificha kutokana na kushindwa kuacha fedha nyumbani.
Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Simanjiro, Thomas Yohana amesema wananchi wasitishwe na propaganda kuwa wakichagua upinzani hawatapatiwa maendeleo.
Yohana amesema kwa muda wa miaka mitano iliyopita kata ya Mirerani haikuwa na shule ya sekondari ila wakaweza kuanzisha na hadi sasa wanafunzi wanasoma hapo japokuwa Chadema ilikuwa inaongoza eneo hilo.
Mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha) Kaanael Minja amesema serikali ya Chadema ikiingia madarakani suala la wanawake kudhalilishwa wakati wa upekuzi wa madini litakwisha.
“Siwezi kuchunguliwa na watoto wangu wakati nikipekuliwa nikitoka machimboni hivyo tuichague Chadema ili kuondokana na udhalilishaji huu,” amesema Minja.