Mratibu wa mashindano ya mbio za magari, Iringa Rally 2020, Hidaya Kamanga akizungumza na wanahabari juu ya mashindano hayo.
Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Iringa, Yusuph Kamota katikati akizungumza kuhusu usalama katika mashindano hayo.
Tawakali ambaye ni Meneja masoko wa Camel Flour akizungumza juu ya udhamini wa Unga wa ngano na udhamini wao kwenye mashindano.
…………………………………………………….
NA DENIS MLOWE, IRINGA
MASHINDANO ya mbio za magari ya ya Iringa Rally 2020 yanatarajia kutimua vumbi mjini Iringa Septemba 19 na kushirikisha timu zipatazo 19 kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Akizungumza na Wanahabari mkoani Iringa Msimamizi wa Mashindano ya Iringa Rally, Hidaya Kamanga alisema maandalizi ya mashindano hayo yamekwisha kamilika kwa asilimia 95 ambapo hadi kufika siku ya tukio maandalizi yote yatakuwa yamekwisha kamilika.
Alisema kuwa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo imejipanga kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ukamilifu na kuleta Burudani kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa ambapo yamekuwa yakileta msisimko kwa mashabiki wa mbio za magari.
Alisema kuwa washiriki mbalimbali 19 wamekwishakamilisha taratibu zote za kushiriki mashindano hayo ambayo yamedhaminiwa na makampuni mbalimbali na wadau wa mbio za magari ambapo madereva wengi waliothibitisha hadi sasa wanatoka Tanzania, akiwemo bingwa wa mashindano hayo mwaka jana Ahmed Huwel ambaye amepania kwa kiasi kikubwa kuibuka bingwa wa mashindano hayo msimu huu.
Aliwataja madereva wanaotarajia kushiriki mashindano hayo kuwa ni Randeep Sigh amnbaye atashirikiana na Zubairy Paredina kutoka timu ya Bird Rally, Gurpa Sandhu na Dave Sihoka kutoka timu ya AESL Racing, Manveer Bird na Ravi Chana kutoka Birdi rally Team, kutoka Siera Zullu team ni Altaf Munge na Ally Hamoud.
Wengine watakaoshiriki mashindano hayo ni kutoka timu ya Munge rally Team,Tylor Rally Team, Juakali Rally Team, TRT/Juakali rally Team,Hari Singh Team A, Hari rally Team B, Hari Rally Team C, Mkwawa Rally Team na Siera Zullu Team.
Team nyingine ambazo zitashiriki mashindano hayo, ni Vulaa rally Team, Siera Rally Team B, mshiriki Fayaz Imran Chandu na Mkwawa rally Team chini ya bingwa wa mashindano hayo Ahmed Huwel akishirikiana na Rahim Suleiman.
Mashindano hayo yanatarajia kuwa ya aina yake kutokana na maandalizi yake kuwa mazuri na wananchi kuyasubiri kwa hamu katika njia yatakayopita ambazo safari hii yataanzia kwenye kituo cha mafuta cha Hope kisha kwenye hotel ya kitalii ya Mount Royal ambapo yatahusisha km 105.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mashindano hayo, Amjad Khan aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo ila kuwa makini na zaidi kwani mashindano ni mashindano na magari yanaweza kukosea njia hivyo si vizuri kukaa jirani na barabara badala yake kuchukua tahadhari wakati wa kushuhudia mbio hizo za magari .
Aidha Khan alisema kuwa unapokuwa kwenye eneo la njia zinapofanyika mbio za magari kuwa makini, mwangalifu kwani waandaaji hawatakuwa na dhamana yoyote pindi ikitokea ajali kwa wananchi hao.
Aliongeza kuwa mtu yoyote hatakiwi kwenda na mtoto katika mashindano hayo na mama mjamzito hawaruhusiwi kuangalia mashindano hayo na wananchi kuwa makini katika maeneo ya kona ambapo gari zinapita
Naye Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa, Yusuph Kamota aliwataka wananchi kuwa makini na mashindano hayo kwani ni hatari endapo itatokea ajali wakati wa mashindano na kuongeza kuwa mashindano hayo ni burudani kama zilivyo nyingine ila ni muhimu kwa wananchi kuwa makini.
Kamota alisema kuwa jeshi la polisi mkoani hapa limejipanga vyema katika kuimarisha ulinzi na Usalama katika Mashindano hayo ili yaweze kumalizika salama na kuwatakia mashindano mema washiriki wa mashindano hayo makubwa kabisa nchini.
Mashindano hayo yanadhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Hotel ya Mount Royal Iringa na mdhamini wa mashindano hayo miaka ya nyuma Maji ya Mkwawa, Camel Unga wa Ngano, Mgahawa wa The Koffee Shop, Kampuni ya Famari, Sunset Hotel, Sai Villa Hotel, Tosti, Alawi Mdee, Azam Tv, na Planet 2000 computer