Home Mchanganyiko TANZANIA YATEULIWA KUWA MJUMBE WA KAMATI YA HATI ZA UTAMBULISHO BARAZA KUU...

TANZANIA YATEULIWA KUWA MJUMBE WA KAMATI YA HATI ZA UTAMBULISHO BARAZA KUU UMOJA WA MATAIFA

0

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeteuliwa kuwa miongoni mwa nchi tisa (9) za wajumbe wanaounda kamati ya Hati za Utambulisho ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Prof. Gaston Kennedy amesema kuwa pamoja na mambo mengine, kamati hiyo ya hati za utambulisho kazi yake kubwa ni kupitia na kujiridhisha juu ya hati zote za wawakilishi wa nchi wananchama wa Umoja wa Mataifa walioteuliwa na Baraza hilo baada ya kupendekezwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Kuteuliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kamati hiyo ni ishara nyingine inayoonesha namna ambavyo Umoja wa Mataifa una imani kubwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na pia nchi wanachama wanavyoiamini Tanzania katika kutekeleza misingi mikubwa ya umoja huo ambayo ni masuala ya ulinzi na usalama, haki za binadamu na utawala bora pamoja na maendeleo. 

Hii ni mara ya tatu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuteuliwa kuingia katika kamati hiyo inayojishughulisha na masauala ya hati za utambulisho ambapo mara ya kwanza ilikuwa katika Baraza la 64 la Mwaka 2009, mara ya pili ilikuwa katika Baraza la 68 la Mwaka 2013 na mara ya tatu Mwaka 2020. 

Nchi nyingine zilizoteuliwa katika kamati hiyo mbali na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Cameroon, China, Iceland, Papua New Guinea, Urusi, Trinidad na Tobago, Marekani na Uruguay.