Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa miwani) akiwaongoza wafugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kuzindua zoezi la uhimilishaji (kupandikiza ng’ombe mimba kwa njia ya mrija).
Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael akizungumzia kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya na namna wizara inayoshirikiana na wananchi ili kuhakikisha wanapata mifugo bora.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Bi. Rahabu Galahenga ambaye amehitimu diploma ya sheria. Prof. Gabriel amefika katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa ajili ya kuzindua kambi ya uhimilishaji.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama katikati), akiwa na wasichana wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya waliohitimu masomo kutoka vyuo mbalimbali nchini. Kutoka kulia ni Bi. Naishiye Eliakimu amehitimu shahada ya ualimu, Bi. Naumu Silomi amehitimu diploma ya uhandisi wa ndege, Bi. Rahabu Galahenga amehitimu diploma ya sheria na Bi. Hawa Julius amehitimu diploma ya ualimu.Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akimpongeza mfugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, baada ya ng’ombe wake kufanyiwa vipimo kwa ajili ya kufanyiwa uhimilishaji.
********************************
Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amesema serikali imelenga kuhakikisha wafugaji nchini wanakuwa na ng’ombe bora, wenye kutoa nyama bora na maziwa mengi wanaopatikana kwa njia ya uhimilishaji (kumpatia ng’ombe mimba kwa njia ya mrija).
Prof. Gabriel amesema hayo katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati akizindua rasmi kambi ya uhimilishaji katika kijiji hicho kwa wafugaji wa jamii ya kimasai na kuwataka waache kufuga kwa mazoea bali wawe na ng’ombe bora na wenye tija huku akiwalenga zaidi akinamama nchini kujikita katika ufugaji wa kisasa.
“Haya ni mafanikio makubwa niwaombe akinamama wengine Tanzania waige mfano wa kina mama wenzano wa jamii ya kimasai walioamua kufuga kisasa kwa kuwa na ng’ombe bora hatuwezi kuendelea kwenye ufugaji wa zamani lazima tufuge kisasa na uhimilishaji unafanyika kwa ng’ombe yeyote hata wa kienyeji.” Amesema Prof. Gabriel
Prof. Gabriel akizungumzia faida za uhimilishaji amesema njia hiyo ya kumpatia ng’ombe mimba kwa njia ya mrija ni muhimu katika kuendeleza ubora wa mifugo hiyo ili kutengenzea mbari na kosaafu bora ya ng’ombe.
Amefafanua kuwa uhimilishaji ni muhimu kwa kuwa mfugaji anaweza kuchagua ng’ombe anayemtaka na ubora wake pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo hiyo kwa ng’ombe dume kupanda ng’ombe wengi kwa wakati mmoja.
Ili kutoa hamasa kwa wafugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Katibu Mkuu Wizara Mifugo na Uvuvi amesema wafugaji watakaohimilisha ng’ombe elfu moja wa mwanzo wizara itagharamia kama sehemu ya uzinduzi na uimarishaji wa kambi za uhimilishaji.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo Bw. Stephen Michael amesema wizara imekuwa ikifanya kazi karibu na wananchi hali iliyofikia kuweka kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha Matebete na kuwafanyia ng’ombe vipimo kabla ya kupandikizwa mbegu.
Naye Afisa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Fadhil Chamwazi ameongeza kuwa kambi za uhimilishaji zina malengo ya kuhamasisha wafugaji kutumia huduma ya uhimilishaji na kuwajengea uwezo jamii ya wafugaji na wataalam juu ya faida ya uhimilishaji.
Bw. Chamwazi amesema zoezi hilo limeanza katika mwaka wa fedha 2019/20 na kwa mwaka 2020/2021 limezinduliwa mkoani Tabora na sasa katika Mkoa wa Mbeya katika Kijiji cha Matebete na kubainisha kuwa vigezo vinavyoangaliwa kwa ng’ombe kabla ya kupandikizwa mbegu ya uzazi kwa njia ya mrija, wataalamu wanakagua afya ya ng’ombe pamoja na kuzingatia umri na muonekano wake.
Nao baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimasai katika kijiji hicho wamefurahishwa na zoezi hilo na kuiomba serikali kuendelea kuwapatia elimu zaidi na kuwafahamisha namna bora zaidi za ufugaji wa ng’ombe bora wa kisasa ili waweze kupata matokeo chanya katika ufugaji wao.