Home Mchanganyiko Tamko la THBUB wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia,...

Tamko la THBUB wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, Septemba 15, 2020

0

******************************

LEO Septemba15, 2020 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote wa demokrasia duniani katika kuadhimisha “Siku ya Kimataifa ya Demokrasia” – “International Day of Democracy.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha siku hii Novemba 8, 2007 ili kuzikumbusha Serikali juu ya wajibu wake wa kukuza na kudumisha demokrasia na kuongeza uelewa wa umma kuhusu suala hilo. Tanzania ikiwa ni mwanachama hai wa umoja huo inao wajibu wa kutekeleza Azimio hilo kwa vitendo. Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “COVID-19: Inavyoangazia Demokrasia.”

 

Kauli mbiu hii imelenga kuzikumbusha nchi wanachama juu ya umuhimu wa kuimarisha mapambano dhidi ya gonjwa hatari la COVID-19 ambalo ni tishio siyo tu kwa afya ya jamii bali pia ushiriki wao katika utawala wa nchi, hususan wakati wa kipindi cha uchaguzi ambacho kinahusisha mikusanyiko mbalimbali ya wananchi.

Wakati siku hii ikiadhimishwa leo, Tanzania inaendelea katika hatua ya kuhakikisha wananchi wanashiriki katika kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wao katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Octoba, 2020.  Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapenda kuipongeza kwa dhati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa Corona 19 na hivyo kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika hatua zote za uchaguzi huo.

Aidha, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inachukua fursa hii kuwakumbusha wananchi na wadau mbalimbali kuwa maradhi ya Corona 19 bado ni tishio katika nchi mbali mbali duniani hivyo wana wajibu kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.

Kwa namna ya kipekee, Tume inawahimiza wananchi kushiriki katika mikutano na majadiliano mbali mbali ya kampeni na kusikiliza sera za viongozi ili kufanya uamuzi unaofaa kwa maendeleo ya Taifa letu.  Aidha Tume inawaasa viongozi kutumia majukwaa ya kampeni kunadi sera zao na kujiepusha na lugha za matusi na zenye kuhatarisha amani ya nchi yetu.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapenda kuwakumbusha wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Imetolewa na:

(SIGNED)

Mohamed Khamis Hamad

Makamu Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

 

15 Septemba, 2020