………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM), Anthony Mavunde ameendelea kuchanja mbuga kwenye kampeni zake huku akitoa ahadi mbalimbali kwa wananchi wa jimbo hilo ikiwemo kukuza zao la zabibu kwa kutafuta masoko ya uhakika.
Akizungumza leo katika mkutano wa kampeni kata ya Mpunguzi ambayo ni maarufu kwa kilimo cha zabibu, Mavunde amesema kama akichaguliwa atatafuta masoko na kuwawezesha akina mama na vijana kuchakata zabibu na kuuza mchuzi wa zabibu.
“Ili kuondokana na zabibu kuoza mashambani nikichaguliwa nitahakikisha nawawezesha vijana na akina mama kuchakata na kuuza mchuzi wa zabibu, kama mnavyojua zabibu yetu inasifika kimataifa kutokana na ubora wake, hivyo kuchakata kutaongeza tija kwenye kilimo hichi, na itakuwa faida kwa wakulima,”amesema.
Amesema atahakikisha anawawezesha wakulima wa nyanya kupata mikopo ili kuongeza tija kwenye uzalishaji na uchakataji wa nyanya.
Kuhusu ujenzi wa shule, Mavunde ameahidi kukamilisha ujenzi wa Shule ya Sekondari mpya ya Nkulabi iliyoanza kujengwa na yeye akishirikiana na wananchi mwaka jana alipokuwa Mbunge wa jimbo hilo.
“Pia mkinichagua tutaanza ujenzi wa Shule ya Msingi mpya eneo la Mlangwa ili kupunguza kero ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu,”amesema.
Kadhalika, amesema katika sekta ya maji na umeme atakamilisha miundombinu ya miradi ya maji Mpunguzi B na Nkulabi na kusimamia usambazaji wa umeme katika maeneo machache yaliyosalia.
“Nitaendelea kukuza michezo na sanaa kwa kufadhili mashindano mbalimbali kwa lengo la kukuza vipaji,”amesema.
&&&&&