Wanafunzi wa shule ya msingi Loorng’swani Kata ya Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa na bango la pongezi baada ya shirika la ECLAT Development Foundation kukabidhi miradi ya thamani ya shilingi milioni 62 ikiwemo madarasa mawili, madawati 46 na matundu 16 ya vyoo, madaftari, kalamu, rula na vifutio.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi (kushoto) akikabidhiwa na Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Development Foundation, Peter Toima Kiroya, hati ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa mawili, madawati 46 na matundu 16 ya vyoo vya shule ya msingi Loorng’swani Kata ya Terrat yenye thamani ya shilingi milioni 62.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Yefred Myenzi (wapili kushoto) akikata utepe kuzindua madarasa mawili, madawati 46 na matundu 16 ya vyoo vya shule ya msingi Loorng’swani Kata ya Terrat, kazi iliyofanywa na shirika la ECLAT Development Foundation.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi akizungumza wakati akikabidhiwa miundombinu ya shule ya msingi Loorng’swani Kata ya Terrat ikiwemo madarasa mawili, madawati 46 na matundu 16 ya vyoo iliyowezeshwa na shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Development Foundation.
…………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la kiserikali la ECLAT Development Foundation limekabidhi miradi ya maendeleo ya thamani ya shilingi milioni 62 ikiwemo madarasa mawili, madawati 46 na matundu 16 ya vyoo vya shule ya msingi Loorng’swani Kata ya Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Mwenyekiti wa ECLAT Foundation Peter Toima akikabidhi miradi hiyo ya shule ya msingi Loorng’swani kwa serikali amesema mradi huo ulianza Februari 20 mwaka huu na kukamilika Septemba 11 kutokana na janga la covid 19.
Toima amesema shirika hilo limechagua vipaumbele vya kimkakati ili kuwawezesha watu waliopo maeneo ya changamoto kupata fursa sawa na watu wa jamii nyingine ili kuinua hali ya maisha yao.
“Nawashukuru wafadhili wetu shirika la Ujerumani la Upendo kwa fedha walizozitoa shilingi milioni 62 na wasimamizi wetu, meneja miradi Bakiri Angalia akisaidiwa na Mosses Kiroya,” amesema Toima.
Amesema shirika hilo lina maeneo matatu ya kipaumbele ya miradi ya uboreshaji miundombinu ya elimu, miradi ya maji na uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi amewataka wanafunzi, walimu, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutunza mradi huo.
Myenzi amewapongeza viongozi wa ECLAT Foundation kwa kufanikisha mradi huo kwani wamekuwa wanatoa kipaumbele kwa jamii ya Simanjiro katika kuchochea maendeleo ya elimu.
“Mngeweza kupeleka mradi huu sehemu nyingine au fedha hizo mkazitumia kwa faida yenu lakini mmeona umuhimu wa kuwekeza kwenye elimu ya jamii ya Simanjiro,” amesema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Terrat, Kone Mendukenya amesema shule hiyo ina wanafunzi 542, wakiwemo wavulana 328 na wasichana 214.
Mendukenya amesema shule hiyo ina madarasa 10 mapungufu mawili, nyumba ya walimu moja pungufu tisa, viti sita mapungufu 140 na viti sita pungufu 14.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Loorng’swani Japhari Sombi amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 125.
Mwalimu Solombi amesema wana imani shirika la ECLAT Foundation wataendelea kutoa ushirikiano ili kuwasaidia zaidi kwani bado wanahitaji msaada zaidi.