MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara Simba SC wameshindwa kutamba ugenini baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Simba walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Muzamil Yassin dakika ya 45 akiiadhibu timu yake ya zamani kwa shuti kali kutoka upande wa kulia wa Uwanja ambalo kipa Mzanzibar, Abdultwalib Mshery alilitemea nyavuni.
Hadi timu zote zinakwenda mapumziko Simba walikuwa mbele kwa bao hilo moja na kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku zikifanya mabadiliko.
Mtibwa Sugar walisawazisha bao kipindi cha pili dakika ya 46 kupitia kwa kiungo mshambuliaji, Boban Zilintusa aliyemchambua kwa kichwa kipa Aishi Salum Manula.
Kwa Matokeo hayo Simba wamefikisha pointi 4 mara baada ya kushinda mechi ya kwanza 2-1 dhidi ya Ihefu huku Mtibwa wakiwa na Pointi 2 baada ya kutoka sare mechi ya kwanza na Ruvu Shooting.
Mechi nyingine za leo, Dodoma Jiji FC imeichapa 2-0 JKT Tanzania mabao ya Jamal Mtegeta dakika ya 50 na Dickson Ambundo dakika ya 80 Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
KMC ikiizamisha mbao 2-1 timu ya Tanzania Prisons ya Mbeya Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu; Ihefu itawakaribisha Ruvu Shooting kuanzia Saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, Biashara United watamenyana na Mwadui FC kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Karume Musoma mkoani Mara na baadaye Saa 1:00 usiku, vigogo Yanga SC watamenyana na Mbeya City Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja tu wa kukamilisha Raundi ya pili, Namungo FC wakiwaalika Polisi Tanzania kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.