…………………………………………………………………
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ilemela kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt Angeline Mabula ameahidi kuboresha na kuimarisha sekta ya uvuvi kwa kusimamia kutengwa kwa kiasi cha shilingi milioni mia mbili na hamsini zitakazotumika kwaajili ya uboreshaji wa mialo ya Samaki ya Mihama, Kayenze na Igombe ili kukuza uchumi na kumaliza tatizo la upatikanaji wa ajira hususani kwa vijana.
Dkt Mabula aliyasema hayo wakati akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho na wananchi waliojitokeza kuhudhuria mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Mihama kata ya Kitangiri ambapo amesema kuwa katika kipindi cha awamu iliyopita mbali na shughuli za kimaendeleo zilizotekelezwa katika sekta ya Uvuvi ikiwemo ujenzi wa mzani wa kisasa wa upimaji wa mazao ya Samaki Kirumba, utoaji wa elimu ya ujasiriamali, utoaji wa mikopo, aliisimamia Serikali kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kinatengwa hivyo kuomba ridhaa kwa wananchi wamchague tena ili akakamilishe utekelezaji wa mradi huo utakaokuwa na manufaa makubwa kwa wavuvi na kuongeza mapato kwa Serikali
‘.. Ninatambua eneo la Mihama idadi kubwa ya wananchi wake ni wavuvi, Tuchague Mimi kuwa mbunge wenu, Rais Mhe Magufuli na diwani wa CCM twende tukaendeleze sekta ya uvuvi, Tushatenga fedha kilichobaki ni usimamizi tu ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula akaongeza kuwa upo mpango mkakati wa kuhakikisha mwalo wa Kirumba nao unafanyiwa maendelezo kwa kutenganisha sehemu ya abiria na sehemu ya kushushia mazao ya Samaki jambo ambalo lilikuwa kero na usumbufu kwa wananchi wanaotumia mwalo huo katika shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wake meneja kampeni wa mbunge huyo, Ndugu Kazungu Idebe akawataka wananchi waliohudhuria mkutano huo kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi na kuchagua wagombea wake kwa nafasi zote za Urais, Ubunge na Udiwani huku akiwakumbusha michango iliyotolewa na mbunge huyo katika kipindi cha awamu iliyopita kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezeka ndani ya kata hiyo ikiwemo ujenzi wa vyumba 89 vya madarasa, ufungaji wa mifumo ya maji na umeme kwa shule za kitangiri na mwinuko uliogharimu jumla ya shilingi milioni mbili.
Kampeni za Mgombea Ubunge huyo zitaendelea leo katika viwanja vya Nyakato Sokoni.