Mratibu wa Vijana Taifa, Padri Adolof Minga (wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa Viwawa Taifa, Leonard Kimu (katikati) wakimkabidhi kiroba cha mchele Padri Thom Rayn Mkuu wa Kituo cha kulelea watoto wenye mtindio wa ubongo na walemavu cha Rehebiltation Centre kikichopo Siuyu mkoani Singida mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mtunza Fedha wa Viwawa Taifa, Bernad Shayo na kushoto ni Mlezi wa Viwawa Jimbo Katoliki Singida, Padri Stefano Sinda.
Mwenyekiti wa Viwawa Taifa, Leonard Kimu, akimkabidhi fedha padri Rayn zilizotolewa na vijana hao kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kituo hicho.
Watoto wakiwa kwenye kituo hicho.
Padri Thom Rayn akiwashukuru vijana hao kwa msaada huo.
Mratibu wa Vijana Taifa, Padri Adolof Minga, akizungumza wakati wakutoa msaada huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
VIJANA Wafanyakazi Wakatoliki (VIWAWA) wamepata viongozi wao wa kitaifa baada ya kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano wa halmashauri kuu uliofanyika mwishoni mwa wiki hii mkoani hapa.
Viongozi hao wapya waliochaguliwa na viongozi wa Viwawa kutoka majimbo ya Kanisa Katoliki ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu ni Mwenyekiti Leonard Kimu kutoka Jimbo Katoliki Singida , Makamu Mwenyekiti Peter Woisso kutoka Jimbo Katoliki Tanga, Katibu Benedict Augustine kutoka Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Katibu Msaidizi Antonia Nyangalima kutoka Jimbo Katoliki Njombe , Mhasibu Bernad Shayo kutoka Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mjumbe Joyce Kimario kutoka Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Akizungumza na vijana hao katika Misa Takatifu ya kuwasimika ambayo iliongozwa na Mratibu wa Vijana Taifa, Padri Adolof Minga aliwataka vijana hao kwenda kutangaza amani katika majimbo yao na kuanzisha miradi ya ufugaji na kilimo ili waweze kujitegemea kiuchumi na kuondokana na utegemezi.
“Ninyi vijana ndio nguzo ya kanisa nendeni mkafanye utume wa kulijenga kanisa letu Katoliki kwa kuwaunganisha vijana wenzenu ambao wapo nje ya kanisa” alisema Minga.
Katika hatua nyingine vijana hao baada ya kusimikwa walikwenda kuwatembelea na kuwafariji watoto wenye mtindio wa ubongo na walemavu wanaolelewa katika Kituo cha Rehebiltation Centre kikichopo Siuyu nje kidogo ya Manispaa ya Singida na kuwapa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mchele, sabuni, maji, pipi, biskuti na vinywaji.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Kituo hicho Padri Thom Rayn aliwashukuru vijana hao kwa moyo huo wa kitume kwa kwenda kuwa fariji watoto hao.
Alisema kituo hicho chenye watoto kati ya 40 na 46 kilianzishwa mwaka 2007 na kinalea watoto wa dini zote pasipo kuwabagua na kuwa shughuli nyingi zinafanywa kwa kujitolea.
Alisema wapo watoto wa shule ya awali hadi darasa la saba na kuwa wamekuwa wakiwafundisha kujitegemea zaidi kama kunawa, kufua, kufanya kazi za bustani kwa kusaidiwa na Sister Rose.
Alisema watoto ambao wanafikisha umri kati ya miaka 15 hadi 16 ambao wanaonesha kuwa na uwezo huwa wanawahamishia kituo chao kingine ambacho kipo Ilongero ambapo ufundishwa ufundi wa kushona nguo, uselemara, upishi lengo likiwa ni waweze kujitegemea.
“Watoto wengi tulionao hapa wanatoka maeneo ya Mbulu Manyara, Dodoma na Singida na hiyo imechangiwa na changamoto ya usafiri kwani hapo awali walikuwa wakitoka mikoa mbalimbali ikiwepo Dar es Salaam.
Mwanafunzi Moses Matesi kwa niaba ya wenzake aliwashukuru vijana hao kwa msaada huo ambao umewapa faraja na kujiona kama watoto wengine ambao wanaishi na familia zao.