Home Siasa DKT.MAGUFULI AAHIDI NEEMA KWA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI

DKT.MAGUFULI AAHIDI NEEMA KWA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI

0

    

Mgombea wa Urais kupitia Tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM, Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia Wananchi wa Katoro katika mkutano wa Kampeni za CCM wakati akielekea Chato mkoani Geita leo tarehe 9 Septemba 2020.

…………………………………………………………

NA JOHN BUKUKU, Geita

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli, amesema akipewa tena ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mitano mingine, Serikali yake itaendelea kuwajali wachimbaji wadogo wa madini nchini wakiwamo wa Geita, kujenga miundombinu ya barabara za lami na kuifungua zaidi nchi kwenye Sekta ya utalii.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo mjini Geita , katika Uwanja wa Kalangalala, ambako mulifanyika mkutano mkubwa wa kampeni za CCM, mkutano ambao ulikuwa ni mkubwa na kuacha simulizi mkoani humo kufuatia maelfu ya wananchi kujitokeza licha ya kufanyika asubuhi muda ambao ni wa kazi.

Dk. Magufuli amesema kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya 2020/2025, wachimbaji wadogo wa madini wataendelea kupewa kwa wingi leseni za uchimbaji, kutengewa maeneo mengi ya uchimbaji, watapewa mafunzo ya uchimbaji, mitaji na teknolojia itakayowawezesha kupata utajiri na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Ilani hiyo  inaeleza kila kitu kama ushahidi kwa wananchi kuhusu mengi ambayo Chama kitaisimamia Serikali kuhakikisha yanafanyika kwa muda wa miaka mitano.

“Haya tumeyaweka katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ukurasa wa 108 hadi ukurasa wa 110 na ndio  maana ninawaomba mtuchague ili haya tuliyoyapanga, yasije yakapotelea hewani, mnufaike nayo,” alisema Dk. Magufuli.

“Serikali imepanga kuhakikisha wachimbaji wadogo wananufaika zaidi na katika hili, tumepanga kuongeza maeneo ya wachimbaji wadogo, tutaendelea kuwapatia leseni, lakini pia mafunzo, mitaji na teknolojia rahisi ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na tija zaidi.

Akizungumzia Utalii, amesema Serikali itaendelea kufungua nchi kwa kuanzisha maeneo ya utalii kwenye kanda zote, kama ambavyo imefanyika Geita, ambako kulikuwa na hifadhi moja ya Rubondo lakini sasa ipo nyingine kubwa ya Burigi-Chato ambayo ni ya tatu kwa ukubwa nchini.

“Tunataka haya maeneo ya kanda ya ziwa, utalii ufanane na ule wa Kaskazini, tunataka maeneo ya kusini Mbeya, Iringa nayo yafanane utalii hivyo hivyo na kwingine, ndio maana tunajenga Uwanja wa Mwanza, mtalii akija moja kwa moja, anapita daraja la kilomita 3.2 la Busisi-Kigongo, anapita Sengerema kwa lami, kisha anamua sasa aende wapi,” amesema.

Alisema uamuzi huo umechukuliwa kuondoa dhana iliyokuwepo awali nchini ya kwamba utalii ni kaskazini pekee, mkoa wa Arusha au Kilimanjaro, kwa lengo la kufungua fursa zinazotokana na sekta hiyo kwa Watanzania wote.

Dk. Magufuli amewaomba wana Geita wawe tayari kwa kupokea watalii, kwa kujenga hoteli za kitalii na kujifunza kupika vyakula vitakavyotumiwa na watalii watakaofika ukanda huo, ili fedha zinazotokana na utalii ziongezeke kutoka dola bilioni 2.6 zilizopo sasa, ambazo zinazalisha ajira milioni 4.

Katika miundombinu, amesema barabara zenye urefu wa kilomita 123, zimejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 212.67, huku mpango ukiwa ni kuendelea kujenga miundombinu hiyo nchi nzima ikiwemo barabara ya Geita- Bukoli- Kahama itakayojengwa kwa kiwango cha lami.

Amesema kwenye viwanda na huduma zingine za jamii, kasi itakuwa zaidi ya iliyokuwepo kwenye miaka mitano ya uongozi wake, ambapo jumla ya viwanda 926 vilianzishwa mkoani Geita.