Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani(kushoto) Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said wakiwa kwenye kikao Pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka TANESCO(hawapo pichani) kabla ya kuanza kwa ukaguzi wa ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere(JNHPP)
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani(mwenye shati la bluu) Naibu Waziri wa Ujenzi wa Misri, Jenerali Mahmoud Nassar,(mwenye suti) wakiwa na wataalamu mbalimbali kutoka nchini Tanzania na Misri wakiangalia picha mbalimbali za Mradi mkubwa wa kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere(JNHPP)
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani(aliyesimama) akizungumza kwenye kikao baina ya ujumbe kutoka Serikali ya Tanzania na Misri kabla ya kuanza kwa ukaguzi wa ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere(JNHPP),Septemba 6,2020.(kushoto) Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said(kulia) Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco Dkt Alexander Kyaruzi.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said(kulia) Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Edward Ishengoma wakiwa katika kikao baina ya ujumbe kutoka Serikali ya Tanzania na Misri kabla ya kuanza kwa ukaguzi wa ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere(JNHPP),Septemba 6,2020.
Naibu Waziri wa Ujenzi wa Misri, Jenerali Mahmoud Nassar akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza kukagua wa ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere(JNHPP),Septemba 6,2020.(kulia) Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.
Ujumbe kutoka katika Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na ujumbe kutoka nchini Misri wakiongozwa na Naibu Waziri wa Ujenzi wa Misri, Jenerali Mahmoud Nassar wakikagua maeneo mbalimbali ya ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere(JNHPP)
…………………………………………………..
Hafsa Omar-Morogoro
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amesema ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere(JNHPP) utakamilika kwa wakati na kwa kiwango cha kimataifa.
Ameyasema hayo, Septemba 6,2020, wakati alipofanya ziara ya ukagua wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa kwenye mto Rufiji.
Katika ziara yake hiyo, aliambatana na Naibu Waziri wa Ujenzi wa Misri,Jenerali Mahmoud Nassar, Katiku Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Edward Ishengoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco Dkt Alexander Kyaruzi, Mkurugenzi Mtendaji Tanesco Dkt Tito Mwinuka na wataalamu mbalimbali kutoka nchini Tanzania na Misri.
Aidha,ameeleza kuwa tayari Serikali imemlipa mkandarasi wa mradi huo zaidi ya trilioni 1.49, ambayo ni sawa na asilimia 100 ya malipo ambayo mkandarasi huyo analitakiwa kulipwa kwasasa, ili kuhakikisha anafanya kazi kwa kasi na kwa kiwango cha kimataifa.
“Tunataka mradi ukamilike kwa wakati na kwa kiwango cha juu, sio mradi unakamilika baada ya miezi miwili unanza kuhitaji tena ukarabati kwa gharama nyengine kwa hili hatutakubali kwahiyo nitoe wito kwa mkandarasi kufanya kazi kwa weledi na kiwango cha juu”alisema.
Amesema kuwa , Serikali imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo, ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda ulipooangwa na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi katika mradi huo.
Katika juhudu za kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, Dkt. Kalemani ametoa maagizo kwa mkandarasi Pamoja na msimamizi wa mradi huo, maagizo hayo ni pamoja na kuwataka waatalamu wote waliofanya kazi kwenye mradi huo kufanya kazi kwa bidii na kumaliza kazi zao kwa wakati.
Pia, amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha kuwa ifikapo mwisho wa mwezi huu awe tayari amemaliza ujenzi wa handaki ujenzi huo ambao ameuelezea kuwa muhimu ambao unategemewa kwa kiasi kikubwa kuendesha mradi huo.
Vilevile, amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anajiri waatalamu wote ambao wanahitajika katika ujenzi wa mradi huo na ifikapo mwisho wa mwezi huo wawe tayari wamefika nchini kwaajili ya ujenzi huo.
“ hatuna wasiwasi na ajira zinazotelewa hapa kwenye mradi hadi sasa umeajiri watanzania zaidi ya 4500 kati ya watanzania 5500 na kwa wale waliobaki waajiri ili kazi ziweze kwenda kwa haraka”alimesema Dkt Kalemani.
Pia, ameagiza uharakishwaji wa ujenzi ya nyumba za wafanyakazi ambazo bado ujenzi wake haujakamilika na kumtaka mkandarasi huyo kuzikamilisha kwa haraka ili wafanyakazi wa mradi huo wahamie katika eneo hilo ambapo itasaidia kufanya kazi zao kwa muda mrefu na mradi huo kukamilika mapema.
Dkt Kalemani, amesema kuwa mradi huo ndio utakaotatua matatizo yote ya umeme nchini na kuahidi Serikali itasimamia kikamilifu ujenzi wa mradi huo ambao utakuwa na faida kubwa na utapunguza changamoto za umeme na utasaidia sana usambazaji wa umeme kwenye vijiji na vitongoji nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi wa Misri, Jenerali Mahmoud Nassar, amesema Rais wa nchi yao anafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo na yupo tayari kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati.
Aidha, amesema kuwa mradi huo utakamilika kwa mafanikio makubwa kwasababu ya ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa Watanzani, na kueeleza kuwa mradi huo utakapokamilika utaleta maendeleo makubwa nchini.
Pia, amesema changamoto zote zilizojitokeza kwenye mradi huo watazifanyia kazi ili kuhakikisha mradi huo unakamika wa kwa muda uliopangwa.
Naye,Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said amesema maendeleo ya mradi huo ni mazuri na changamoto zilizojitokeza zitafanyiwa kazi na kuwataka Watanzania kuendelea kuunga mkono mradi huo wenye faida nyingi katika katika Taifa letu.