Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Rukwa Benjamin Mangwala akitoa nasaha kwa viongozi wa vyama vya ushirika katika kuhakikisha wanazingatia sheria za kuingia mikataba ya mikopo na kampuni za usamabazaji dhana bora za kilimo.
Kaimu Meneja wa Kampuni ya Agricom Africa Remy Lindi akielezea zana za kilimo zinazosambazwa na kampuni hiyo katika mkoa wa Rukwa ili kuwapa fursa wakulima wa mkoa huo kulima kwa tija.
Afisa zana za kilimo mkoa wa Rukwa Mhandisi Sebastian Kioyo akielezea faida za matumizi ya zana bora za kilimo kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika (hawapo pichani) katika uzinduzi wa Programu ya matumizi Bora ya Zana za kilimo mkoa wa Rukwa.
kaimu Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Rukwa Ocran Chengula akijaribu moja ya zana za kilimo zinazosamabazwa na kampuni ya Agricom kujionea ubora wa zana hizo mara tu baada ya mafunzo ya zana hizo.
…………………………………………………………………
Vyama vya Ushirika Mkoani Rukwa vimetakiwa kuwekeza nguvu zao katika upatikanaji wa zana bora za kilimo ili kuweza kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao mbalimbali mkoani Rukwa hasa katika kipindi hiki wanachojiandaa kuanza msimu mpya wa kilimo unaotarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu.
Akiongea wakati wa Ufunguzi wa uzinduzi wa Mkakati wa matumizi bora ya zana za kilimo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Rukwa, Ocran Chengula alisema kuwa, asilimia 80 ya uchumi wa Mkoa wa Rukwa unategemea kilimo lakini ni asilimia 3 tu ya wakulima wanatumia matrekta hali inayopekelea eneo kubwa la ardhi inayofaa kulimwa katika mkoa huo kutolimwa na pia kutopata mazao bora yenye kuhimili ushindani katika soko la dunia.
“Katika mkoa wetu kuna hekta 1,660,000 ambazo zinafaa kwa kilimo, lakini kati ya hizo kwa kiasi kikubwa sana tunazoloma ni hekta laki tano na kidogo, ambazo ni sawa na asilimia 32 kuna kipindi tulifika hadi asilimia 35 lakini ni kiasi kidogo sana, na kitu ambacho kinatukwamisha katika kuongeza eneo la kilimo ni kutumia zana ambazo sio Rafiki kwa kilimo, katika mkoa wetu kwa kiasi kikubwa sana (75%) tunatumia zana za kukokotwa na ng’ombe kwa maana ya maksai,” Alisema.
Wakati akielezea mpango wa serikali kuhakikisha wanavitumia vyama vya ushirika ili kuwawezesha wakulima wadogo wadogo kulima kwa tija, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika mkoani Rukwa Benjamin Mangwala alisema kuwa, Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini imeridhia vyama hivyo kuingia mikataba ya mauziano na matumizi ya zana bora za kilimo na makampuni ya usambazaji wa zana hizo ili kuondokana na matumizi ya zana duni huku akifafanua sheria zitakazolinda mikataba hiyo.
“Hiyo sheria ya Ushirika ya mwaka 2013 inaekeleza kwamba maamuzi ya kuweza kununua hayo matreka yatatokana na maamuzi ya wanachama husika na si vinginevyo kwa maana nyingine ni kwamba pale ambapo azimio litafanyika wakati mahudhurio ya wanachama yapo chini kwa mujibu wa sheria, azimio hilo halitakuwa halali na hivyo chama husika kitaathirika kwa kushindwa kukidhi sifa za hilo azimio, hata kama walikuwa na sifa ya kupata hicho kifaa, hivyo niwaombe viongozi wa vyama vya ushirika na maafisa ushirika mshirikiane,” Alieleza.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa kampuni ya Agricom African Limited Remy Lindi alisema kuwa wameamua kufika mkoani Rukwa baada ya kuona wakulima wengi wanashindwa kulima kwa tija kutofikia malengo kwasababu ya kukosa zana bora za kilimo ambazo kampuni hiyo inaagiza na kuzisambaza kwa wakulima.
“Agricom tumeamua kuja huku na kutoa hii elimu ya utumiaji wa zana hizi bora ili mwisho wa siku waweze kuhama na kubadilika na kuona manufaa kwasababu huwezi kumshawishi mtu kutumia zana pasipokuelewa faida yake, ndio maana tunasema shamba pesa maana yake ni kwamba lazima ufanye vitu kitaalamu na kisasa ili kuweza kupata pesa kutoka shambani,” Alimalizia.
Miongoni mwa wafaidika wa elimu hiyo ya matumizi bora ya zana za kilimo Mwenyekiti wa Kanyele AMCOS Esther Sikozi alisema kuwa, ujio wa vifaa hivyo utawapunguzia kazi kwani ukilimakwa kutumia Wanyama kazi unatumia siku mbili hati tatu kumaliza ekari moja wakati trekta linatumia dakika chache kulima ekari moja.
Mkoa wa Rukwa una vyama vya ushirika 166 huku 88 vikiwa vinajihusisha na kilimo na ni vyama 29 pekee ndivyo vyenye sifa za kukopesheka na hiyo ni baada ya kuvuka kigezo cha kuwa na idadi kadhaa ya wanachama ambao wanaweza kuchangia ili kuweza kulipa mkopo wa trekta la kulimia.
Maelezo ya Picha
DSC_0458 – Baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Rukwa wakipata mafunzo ya matumizi ya dhana bora za kilimo wakati wakijiandaa na msimu mpya wa kilimo.