*************************************
Na John Walter-Babati
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaasa wanaCCM wote waliotia nia ya kugombea ubunge wa Jimbo hilo waondoe tofauti zao na kuwaunga mkono wagombea walioteuliwa na Chama hicho Paulina Gekul Babati mjini na Daniel Sillo Babati vijijini.
Majaliwa aliyazungumza hayo wakati alipokuwa akizindua Kampeni za CCM katika Mkoa wa Manyara kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati.
Jimbo la Babati mini lilikuwa na wagombea zaidi ya 30 ambapo kati ya hao watatu waliwahi kukalia kiti Cha Bunge.
Ester Mahawe ambaye alikuwa Mbunge wa Viti maalum mkoani Manyara aliongoza katika kura zilizopigwa na wajumbe 91 lakini hakupata ridhaa ya kugombea kutoka ngazi ya juu ya chama hicho.
Anna Gidarya alikalia kiti hicho kama Mbunge wa viti maalum akiwa chama kikuu cha Upinzani (CHADEMA) na baadaye bunge lilipovunjwa alihamia Chama Cha Mapinduzi naye aligombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo hilo pamoja na Viti maalum lakini hakufanikiwa kupata kura za kutosha.
Mwingine aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Babati mjini ni Chambiri Werema ambaye alifanikiwa kuwa wa pili kwenye mchakato wa kura za Maoni kwa kwa kupata kura 77.
Paulina Gekul ambaye alikuwa Mbunge wa Chadema na baadaye kuhamia Ccm katika Mchakato wa kura za maoni alipata kura 61 na baadaye baada ya uongozi wa juu kuketi ulirejesha jina lake kugombea nafasi hiyo tena katika Jimbo la Babati mjini.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa akiwa mjini Babati aliwataka wote waliwania nafasi hiyo lakini hawakufanikiwa kupenya, waungane na kuwa kitu kimoja kuzisaka kura ambazo zitakiwezesha chama hicho kuchukua Jimbo.