Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza katika mkutano wa Kampeni za Urais kwa upande wa CCM uliofanyika katika uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga leo tarehe 03 Septemba 2020.
Mgombea Uunge wa jimbo la Shinyanga mjini Bw. Patrobas Katambi akiwaomba kura wananchi wa mji wa Shinyanga katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga leo.
PICHA NA JOHN BUKUKU- SHINYANGA.
……………………………………………..
NA EMMANUEL MBATILO
Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM, Mhe.Dkt.John Pome Magufuli amesema katika miaka mitano ya kumaliza uongozi wake atahakikisha suala la umeme limekamilika nchi nzima kwa kiasi kikubwa hivyo amewataka wananchi wamchague ili kutimiza ahadi zake.
Ameyasema hayo leo akiwahutubia Wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga leo ambapo wananchi wamejitokeza kwa wingi kumsikiliza mgombea huyo kupitia CCM
“Hapa Shinyanga tumetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Hospitali, Zahanati, Barabara, tumekamilisha mradi mkubwa wa kusafirisha umeme kutoka Iringa-Dodoma-Singida hadi Shinyanga, itafika mahali tatizo la umeme litakuwa ni ndoto, vijiji 136 vya Mkoa huu tumepeleka umeme”. Amesema Mhe.Dkt. Magufuli.
Aidha, Mhe.Dkt.Magufuli amesema mambo mengi wameyafanya hasa kutekeleza ahadi walizoahidi kwa wananchi kwa miaka mitano iliyopita.
“Awamu ijayo ni mengi tuliyoahidi kuyatekeleza lakini katika Ilani hii ya CCM imeainisha mengi ya kufanya katika Mkoa huu wa Shinyanga ikiwemo kuboresha zaidi elimu, Afya, miundombinu. Naahidi kuyafanyia kazi kwa ukaribu haya yote tuliyoahidi”.-Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt John Magufuli amesema.
Pamoja na hayo amewashukuru watanzania wote kusimama pamoja katika masuala mbalimbalia hasa katika majanga kama Corona hivyo amewaomba waendelee kuwa pamoja na kumuomba Mungu kulinda taifa.
“Mungu ametenda maajabu kwa Taifa letu na Corona imeisha nawashukuru sana Watanzania wote kwa kusimama pamoja, Shinyanga mmefunika sana na mmejitokeza kwa wingi nimefurahi, miaka mitano iliyopita mliniamini, naomba muendelee kuniamini” – amesema JPM akiwa Shinyanga