…………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,CHALINZE
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Ridhiwani Kikwete, ameahidi kuendelea kusimamia miradi mbalimbali ikiwemo ya kimkakati ambayo bado haijakamilika kwa manufaa ya wanaChalinze pindi akichaguliwa pamoja na madiwani .
Aidha Ridhiwani amewashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuonesha imani yao kwake kwa kumpigia kura za kutosha, huku akiishukuru zaidi Halmashauri Kuu ya chama hicho Taifa chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kupitisha jina lake.
Akizungumza na Waandishi wa habari,Ridhiwani alisema katika kipindi cha miaka mitano Serikali imetelekeza kwa vitendo ilani ya CCM iliyoitoa wakati kikiomba ridhaa kwa wananchi mwaka 2015.
Alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa ndani ya jimbo hilo ni pamoja na ujenzi wa viwanda, umeme, vituo vya afya, hospitali ya Msoga sanjali na maji kupitia mradi mkubwa unaotokea chanzo cha Mto Ruvu utaovinufaisha vijojo na vitongoji mbalimbali mpaka Mboga kiwandani.
“Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambae pia ndio Mwenyekiti Chama Cha Mapinduzi, inatekeleza kwa vitendo utekelezaji wa miradi mikubwa na midogo, hapa Chalinze kuna ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, shule mpya na kukarabatiwa za awali, maji, umeme na miundombinu ya barabara,” alisema Ridhiwani.
Mwenyekiti wa chama hicho wilayani Bagamoyo ,Abdul Sharifu alieleza, CCM imefanya mambo makubwa, na kwamba watakwenda kwenye kampeni wakiwa na miradi mingi ya kuisemea ikiwemo mikubwa na midogo.
Ridhiwani anatetea nafasi hiyo baada ya miaka mitano ya kwanza, iliyotanguliwa na mwaka mmoja wa 2014 kuchaguliwa katika uchaguzi mdogo, uliotokana na kifo cha aliyekuwa anashika nafasi hiyo Said Bwanamdogo.