MSERBIA Zlatko Krmpotic anatarajwa kuwasili nchini kesho kutoka kwao Yugoslavia kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuwa kocha mpya wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.
Krmpotic mwenye umri wa miaka 62, mzaliwa wa Belgrade, ni kocha mwenye uzoefu mkubwa aliyeanzia kwenye kucheza soka katika nafasi ya ulinzi.
Kati ya mwaka 1977 na 1986, Krmpotić aliichezea mechi zaidi ya 200 za mashindano yote klabu ya Red Star Belgrade ya kwao kwa misimu tisa, na kushinda mataji matano.
Baada ya hapo akaenda Uturuki na kuchezea kwa misimu miwili klabu ya Genclerbirligi kati ya 1986 na 1988 kabla ya kurejea nyumbani kwao kumalizia soka yake katika klabu ya AIK Backa Topola.
Krmpotic pia aliichezea timu ya taifa ya Yugoslavia mechi mbili katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1982, timu hiyo ikimaliza kwenye nafasi ya tatu katika Kundi la Tano.
Awali, kocha huyo mpya wa Yanga, Krmpotic alishinda Kombe la Mataifa ya Ulaya kwa vijana chini ya umri wa miaka 21 ‘UEFA Euro U-21’ mwaka 1978 akiwa na Yugoslavia.
Na tangu awe kocha, Krmpotić amefundisha Vilabu tofauti katika nchi 12 duniani, ambazo ni AIK Bačka Topola, OFK Beograd za Serbia, Degerfors IF ya Sweden, Sloga Jugomagnat ya FYR Macedonia, Ankaragücü ya Uturuki, Paniliakos ya Ugiriki, Nea Salamis ya Cyprus, Kairat ya Kazakhstan na Kazma ya Kuwait.
Nyingine ni Don Bosco ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ZESCO United ya Zambia, Jwaneng Galaxy ya Botswana, APR ya Rwanda, Polokwane City na Royal Eagles za Afrika Kusini.
Pia aliziongoza timu za taifa za vijana za Serbia na Montenegro chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2005 na U19 ya Serbia 2007 na 2008.
Krmpotic mwenye uraia wa Croatia amewahi kushinda tuzo za Kocha Bora wa DRC msimu wa 2016-2017, Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Zambia msimu wa 2017-2018, Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Botswana mwaka 2018 na Kocha Bora wa Afrika 2017-2018.
Krmpotic anakuja Yanga SC baada ya mpango wa klabu hiyo kumchukua Mrundi, Cedric Kaze aliyekuwa anafundisha akademi za Barcelona nchini Canada kushindikana kufuatia kuachana na kocha Mbelgiji, Luc Eymael aliyedumu kwa miezi saba tangu Januari.