Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Charles,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi za Tume zilizopo Njedengwa jijini Dodoma akitoa taarifa kwa umma kuhusu vyombo vya habari vinavyotangaza matokeo ya uteuzi wa wagombea wa Ubunge na Udiwani
…………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Charles amesema tume bado haijatoa taarifa yoyote ya kutangaza mgombea wa mbunge au Udiwani ambaye amepitishwa bila kupingwa.
Pia NEC imekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuwa wapo wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani waliopitishwa bila kupingwa.
Kauli ameitoa leo jijini Dodoma katika Ofisi za Tume zilizopo Njedengwa wakati akizungumza na wandishi wa habari .
Aidha Dkt. Charles amesema kuwa hakuna pingamizi lolote lililotolewa kwa wagombea wa Urais wa vyama 15 ambavyo jana vilipitishwa na tume kugombea.
Kwa kuongezea Dkt. Charles amesema haiwezekani wawepo wagombea ambao wamepita bila kupingwa ilihali muda wa kuwekewa mapingamizi ambao kisheria ni kuanzia jana saa kumi jioni baada ya kupitishwa hadi leo saa kumi jioni.
” Kwa mujibu wa kifungu cha 40 (2) cha sheria ya Tume ya Uchaguzi sura ya 343 pingamizi linaweza kuwekwa kwa wagombea wa ubunge kama zuio kwa wagombea aliyeteuliwa kuanzia saa kumi jioni ya siku ya uteuzi hadi saa kumi jioni ya siku inayofuatia baada ya siku ya uteuzi”, ameeleza Dkt. Charles.
“Sasa ni jambo la kushangaza kuona vipo vyombo vya habari ambavyo vinatangaza uwepo wa wagombea waliopitishwa bila kupingwa kabla ya muda wa mapingamizi kuisha, tunawasihi sana ndugu zetu wanahabari kuepusha kutoa taarifa ambazo hazijathibitishwa na tume,” ameeleza Dkt. Charles.
Hata hivyo Dkt.Charles ameviasa vyombo vya habari kuzingatia sheria na maadili ya kazi zao pia Tume itachukua hatua kali za kisheria kwa chombo chochote kitakachoonekana kwenda kinyume na sheria,kanuni na taratibu za Uchaguzi.