Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera akiwa Ofisini kwake
Katika kipindi cha miaka mitano (5) chini ya Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dr. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeshuhudia mengi makubwa yamefanyika katika Wilaya yetu ya Busega ukilinganisha na hapo awali. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera wakati akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake mapema wiki hii.
Akiongea kwa ujumla Mhe. Mwera amesema awamu ya tano imefanya mambo mengi katika nchi yetu kwa ujumla, hiyo imechangiwa na uadilifu wa viongozi wengi wa serikali ya awamu hii ya tano. Mapambano dhidi ya rushwa iliyokithiri, kuimarika kwa ukusanyaji mapato, elimu bila malipo, ujenzi wa miundombinu ya barabara, uwajibikaji wa watumishi ni miongoni mwa mambo makubwa yaliyosimamiwa vyema na Mhe. Magufuli, aliongeza Mhe. Mwera.
Wilaya ya Busega imeweza kutekeleza miradi mingi chini ya serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka mitano. Ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya wilaya ya Busega ambalo linagharimu TZS Bilioni 4.9 ambapo mradi umefikia asilimia 60%. Sambamba na ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri, pia serikali imeweza kujenga jengo la Ofisi ya Mkkuu wa Wilaya ambapo gharama yake ni TZS Bilioni 1.1 na mpaka sasa limefikia asilimia 98%.
Kwa upande wa Afya, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya umegharimu TZS Bilioni 1.8 na huduma zimeanza kutolewa huku baadhi ya miundombinu ikiendelea na ujenzi wake. Licha ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya, pia upanuzi wa vituo vya Afya ili kuboresha huduma za afya Wilayani Busega umetekelezwa na serikali.
Upanuzi wa Vituo vya Afya vya Nassa na Igalukilo kwa TZS. 850 Milioni. Pia serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya imeweza kuboresha miundombinu kwenye vituo vya afya na zahanati kwa gharama ya TZS. Milioni 606.5 katika zahanati za nyamikoma, Mwasamba, Mwanhale, Ijiha, Nyaluhande, Mwamagigisi, badugu, Ngasamo, Kalemela na vituo vya afya vya Kiloleli na Lukungu.
Aidha Mhe. Mwera amesema mapinduzi makubwa yamefanyika Wilayani Busega kwa upande wa elimu mpaka sasa tumepataTZS Bilioni 2.7 kwaajili ya elimu bila malipo wilayani Busega. Hali hii imefanya ufaulu kupanda kwa upande wa shule za msingi kutoka asilimia 73.8% mwaka 2015 mpaka asimilia 90.2% mwaka 2019. Aidha Mhe. Mwera amekiri kupanda kwa ufaulu kwa shule za sekondari kutoka asimilia 58% mwaka 2015 mpaka kufikia asilimia 77% mwaka 2019.
“kwa upande wa elimu tumepanda sana na kwa mwaka jana tumeweza kuingiza wanafunzi wanne kitaifa kwa matokeo ya mtihani wa darasa la saba, sio kitu kidogo kwa wilaya yetu kuingiza watoto wanne kwenye wanafunzi 10 bora kitaifa, kwa hilo tunajivunia sana”, aliongeza Mhe. Mwera.
Pamoja na kuimarika kwa elimu wilayani Busega, pia serikali imeweza kujenga miundombinu ya elimu ili kuchochea upatikanaji wa elimu bora ikiwemo ujenzi wa shule tatu (3) mpya za sekondari katika kipindi cha miaka mitano chini ya serikali ya awamu ya tano. Ujenzi wa shule ya Sekondari ya Dr. Chegeni, shule ya Sekondari Masanza na Shule ya sekondari Antony Mtaka imesaidia kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaojiunga kidato cha kwanza na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani. Ujenzi wa shule hizo mpya 3 za sekondari kumeifanya wilaya kuwa idadi ya shule za sekondari zipatazo 20.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara, serikali imeweza kuboresha na kuongeza mitandao ya barabara wilayani Busega kutoka barabara 36 zenye urefu wa kilomita 326.99 mwaka 2015 mpaka barabara 136 zenye urefu wa kilomita 511.11 mwaka 2020.
Kuanzia mwaka 2015 serikali imeweza kutoa jumla ya fedha zaidi ya TZS Bilioni 4.689 ambapo kati ya hizo zaidi ya TZS 2.39 ni fedha za matengenezo kutoka bodi ya mfuko wa barabara na zaidi ya TZS 2.29 ni fedha za miradi ya maendeleo (MIVARF).
Miundombinu ya maji imetekelezwa kwa ukubwa kwa kipindi cha miaka mitano ikiwemo utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Lamadi wenye thamani ya TZS Bilioni 12.8 ambao umekamilika na tayari unatumika.
Miradi mingine ni pamoja na mradi wa maji Lukungu, mradi wa maji kiloleli, mradi wa maji Badugu, mradi wa maji Nyashimo, mradi wa maji Bushigwamhala na mradi wa maji Busami na jumla ya gharama ya miradi hiyo tajwa kwa ujumla katika kipindi cha miaka 5 kuwa na thamani ya Zaidi ya TZS Bilioni 5.7.
Nishati katika Wilaya ya Busega imekuwa ya kuridhisha huku Mhe. Mwera akiishukuru serikali kwa kunufaika sana na mpango wa usambazaji umeme vijijini (REA). Kutoka mwaka 2015 ni vijiji 24 viliunganishwa na huduma ya umeme kati ya vijiji 59 lakini mpaka kufikia 2020 takribani vijiji 53 vimeunganishwa na huduma ya umeme, hivyo ni vijiji 6 pekee vimesalia kuunganishwa umeme, aliongeza Mhe. Mwera.
Utekelezaji wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) ni miongoni mwa juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wanakua kiuchumi kwa kuongeza kipato.
Wilaya ya Busega imeweza kuwezesha wananchi kwa kupitia vikundi vya Wanawake, Vijana na Walemavu kwa kuwapatia mikopo ya masharti nafuu, huku zaidi ya TZS milioni 188, vikundi vya Wanawake kutoka 26 mwaka 2015/2016 kufikia vikundi 51 mwaka 2019/2020 hivyo kufanya thamani ya mikopo kuwa zaidi ya TZS milioni 86.2, vikundi vya Vijana kutoka 13 mwaka 2015 hadi 23 mwaka 2019/2020 na thamani ya mikopo kuwa zaidi ya TZS milioni 71.6. Halikadhalika utoaji mikopo kwa vikundi vya watu wenye ulemavu umeongezeka kutoka kikundi 1 mwaka 2015/2016 hadi kufikia vikundi 7 mwaka 2019/2020 na kufanya gharama za mikopo kufikia zaidi ya TZS milioni 19.5.
Mpango wa kunusuru kaya masikini, TASAF umeweza kutekelezwa vyema wilayani Busega kwani kuanzia mwaka 2015/2016 mpaka 2019/2020 jumla ya kaya 4180 zimeweza kunufaika na mpango huo ambapo jumla ya TZS Bilioni 3.744 zimetumika.
Serikali imefanya mambo mengi wilayani Busega na kwakweli ni jambo la kumshukuru sana Mhe. Dr. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupendelea sana katika kipindi hiki cha miaka mitano chini ya serikali ya awamu ya tano kwani Busega ya miaka mitano nyuma sio hii ya sasa, alisema Mhe. Mwera.