…………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
BAADA ya kupitishwa na Chama chao cha Mapinduzi (CCM) na kisha kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa leo wagombea wa Ubunge, Deo Ndejembi wa Jimbo la Chamwino na Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ wa Mtera wamerudisha fomu kwa Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Dodoma, Athuman Masasi huku wakipita bila kupingwa.
Wagombea hao wote majimbo yao yapo katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambapo wameahidi kufanya kampeni za kistaarabu huku wakiahidi kushughulika na kero za wananchi.
Akizungumza baada ya kurudisha fomu mgombea wa ubunge Chamwino, Deo Ndejembi amesema anaamini kwa mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Dk John Magufuli ni wazi watapata kura nyingi za ndio kutokana na imani kubwa ambayo serikali imejenga kwa wananchi.
” Nakishukuru chama changu kwa kunipitisha niwaahidi ndugu zangu wa Chamwino kwamba ninakuja kufanya kazi ya kuwatumikia nyinyi, ninakuja kushirikiana na serikali yetu kuwaletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” Amesema Ndejembi.
Kwa upande wake Lusinde amewataka watanzania kumpigia kura nyingi za ndio Rais Magufuli ili kumpa heshima kwa utendaji wake uliovunja rekodi nchini na nje ya Nchi.
” Wananchi wenzangu wa Chamwino ni ahadi yetu kwenu kwamba tuna dhamira ya dhati ya kuwatumikia, mmeona namna ambavyo Rais wetu amefanya kazi kubwa ikiwemo kuifanya Nchi yetu kuwa na uchumi wa kati hata kabla ya 2025 ambapo tulikua tumejiwekea malengo,” Amesema Lusinde.