Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari inayongozwa na Felistas Mushi (Mwenyekiti) kutoka Wizara ya Katiba na Sheria imetembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha.
Kamati hiyo ya watalaamu watano imefika kwa Mkuu wa Mkoa Mh. Idd Hassan Kimanta kujitambulisha kabla ya kuanza utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya Ujenzi wa Amani Nchini katika Mkoa wa Arusha katika maeneo amabayo yamekuwa yakikumbwa na migogoro inayohusisha rasilimali na hatimaye kusababisha mapigano na mauaji kati ya wakulima na wafugaji, wawekezaji na wananchi na wakati mwingine wananchi wenyewe kwa wenyewe.
Kamati hii iliundwa mwezi Februari, 2012 chini ya Itifaki ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyoridhiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mkataba wa nchi za Maziwa Makuu wa Usalama, Utulivu na Maendeleo (The Pact on Security, Stability and Development in the Great Lakes Region).
Wataalamu na Wajumbe katika Kamati hiyo ya Kitaifa ni Pius Katani kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Saleh Ambika wa Wizara ya Mambo ya Ndani (Jeshi la Polisi), Lina Kitosi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Miraji Maira wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambaye pia ni Katibu wa Kamati.