Home Mchanganyiko URASIMISHAJI UTUMIKE KAMA FURSA KUELEKEA UCHUMI WA KATI

URASIMISHAJI UTUMIKE KAMA FURSA KUELEKEA UCHUMI WA KATI

0

Wataalm wa Upimaji kutoka Kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi cha
kutatua changamoto za uramishaji wakihakiki alama za upimaji zilizowekwa
katika Mtaa wa Kambi ya Maziwa, Kata ya Matevesi Mkoani Arusha.

Kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi, kikijadiliana jinsi uwekaji alama za
upimaji (beacons) ulivyowekwa uwandani kulingana na ulivyo kwenye ramani ya
upimaji katita Mtaa wa Kambi ya Maziwa, Kata ya Matevesi Mkoani Arusha.

Kiongozi wa kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi cha kutatua changamoto za
urasimishaji Bwn PrayGod Shao (aliyeshika kamba) akiongoza ukaguzi wa
uwekaji alama za upimaji katika maeneo ya hifadhi ya bararabara ya Arusha –
Moshi katika Kata ya Matevesi Mkoani Arusha.

……………………………………………………………………….
Mratibu wa kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kilichoundwa kwa ajili ya kutatua na kukwamua changamoto za urasimishaji makazi
holela mkoani Arusha Bwn PrayGod Mosha amesema, Urasimishaji ni fursa ambayo
madhumuni yake ni kuinua uchumi wa mwananchi wa hali ya chini. Haya yalibainishwa
katika ukaguzi unaondelea kwenye mitaa mbalimbali ya Mkoa wa Arusha ambayo zoezi
la kurasimisha makazi linaendeshwa na makampuni ya watu binafsi.
Akizungumza na kamati ya urasimishaji katika mtaa wa Kambi ya Maziwa, Kata ya
Matevesi Shao alisema, urasimishaji una faida kubwa kwa mwananchi mmoja mmoja
lakini pia kwa Taifa nzima. Kazi kubwa ya warasimishaji na kamati walizo nazo pamoja
na kusimamia mikataba ya urasimishaji ni pamoja na kutoa elimu ya kutosha kuhusu
umuhimu wa urasimishaji makazi.
Aliongeza kwamba, katika kuelekea uchumi wa kati, wananchi wanatakiwa kuishi katika
maeneo ambayo yamepangwa na kupimwa ili waweze kupata huduma za msingi za
kijamii. Upatikanaji wa huduma za kijamii katika maeneo yanayo wazunguka wananchi
ni fursa kwao kiuchumi.
‘Kama maeneo yakiwa yamepangika na kupimwa vizuri kwenye mitaa, lazima wananchi
watakuwa wanafanya biashara ndogondogo na kujipatia kipato, pia watakuwa na
barabara za kupitisha bidhaa zao endapo watahitaji kuzisafirisha kutoka mtaa mmoja
kwenda mtaa mwingine alisema Shao’.
Aidha, Rubeni Mpanda katibu wa kamati ya urasimishaji mtaa wa Kambi ya Maziwa
alisema, zoezi linaenda vizuri na wananchi wanashirikishwa japo changamoto ni
kwamba baadhi yao hawapatikani kwenye makazi yao wakati wa utekelezaji na hivyo
kulazimisha kazi kufanyika polepole. Mpanda aliongeza kwamba, yeye na viongozi
wenzake wa kamati ya urasimishaji walisahawatembelea wananchi wote ambao bado
hawajawekewa alama za upimaji (beacons) na kuwaomba angalau siku za Jumamosi
na Jumapili washirikiane na warasimishaji ili kuwawekea alama za upimaji katika
maeneo yao lakini hawajafanikiwa bado.
‘Urasimishaji ni lazima uwe zoezi shirikishi ndiyo maana kazi inafanyika taratibu ili kila
mwananchi aridhike na ashiriki katika zoezi la uwekaji alama za upimaji. Malalamiko
mengi yaliyopo ya urasimishaji ni kutoka kwa wale ambao tunawafuatilia na
hawapatikani kwa sababu mwisho wa siku ni lazima kazi iendelee, alisema Mpanda.’
Siku zote wananchi wanaamini ahadi wanazopewa awali katika utambulisho wa mradi.
Matumaini mengi ya wananchi wa Mkoa wa Arusha yalikuwa kuona mradi wa
urasimishaji unatekelezeka kwa wakati. Kuchelewesha utekelezaji kunasababisha
maswali na hofu kwa wananchi ambao walishachangia fedha zao kwenye huo mradi.
Warasimishaji wote katika mkoa wa Arusha wamepewa hadi Agosti 30, mwaka huu

2020 wakamilishe kazi zote za urasimishaji ili wananchi waweze kuandaliwa hati za
umiliki katika maeneo yao.

——————————————————-MWISHO————————————————