………………………………………………..
Joctan Agustino,Njombe
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe, Seleman Jafo Agosti 17/2020 ameweka jiwe la msingi katika Soko jipya na la kisasa lililojengwa Mkoani Njombe ambalo kwa sasa limefikia asilimia tisini na saba za utekelezaji.
Baada ya kukamilika Soko hilo linatarajiwa kutoa fursa kwa zaidi ya wafanyabiashara mia saba huku likikadiriwa kuongeza makusanyo ya mapato ya Halmashauri hadi kufikia million mia tatu kwa mwaka tofauti na soko la awali ambalo lilikuwa likikusanya wastani wa shillingi Million hamsini kwa mwaka.
Pamoja na kuweka Jiwe la Msingi kwenye Soko hilo litakalogharimu Fedha za Kitanzania kiasi cha Shilingi Billion 10.5 hadi kukamilika kwake pia Waziri Jafo amefanya uzinduzi wa mpango kabambe wa matumizi ya Ardhi (Master Plan) katika Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa Mzee Jassel Mwamwala walishiriki Tukio hilo na kushuhudia utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt, John Pombe Magufuli.
Katika Hatua nyingine MHE, Jafo amekabidhi mfano wa hundi ya Makusanyo ya Madeni sugu ya iliyokuwa Benki ya NJOCOBA, SACOSS na AMCOS yenye zaidi ya Fedha za Kitanzania kiasi cha Shilingi Bilioni tano.
Akizungumza kabla ya kukabidhi mfano wa hundi hiyo Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bi, Catalina Revocati alisema fedha hizo zimekusanywa na kikosi kazi kulichoundwa Oktoba 23/2019 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe, Christopher Ole Sendeka.
Mbele ya wakazi wa Mkoa wa Njombe walioshiriki tukio hilo Mkurugenzi wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbung’o alisema wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais ya kukusanya fedha kwa wadaiwa wote Nchini ili fedha hizo zirejeshwe kwa Wananchi.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Seleman Jafo pamoja na Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Bw, Charles Malunde wametoa onyo kwa Watendaji wanaohusika na ukusanyaji wa Fedha hizo kuhakikisha zinarejeshwa na kuwanufaisha walengwa.