Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa Elimu kujenga uelewa wa pamoja kuhusu Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP)uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo na baadhi ya Viongozi wa Sekta ya Elimu wakiwa katika Mkutano wa wadau wa Elimu kujenga uelewa wa pamoja kuhusu Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP)uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa Elimu kujenga uelewa wa pamoja kuhusu Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP)uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Gerald Mweli akizungumza wakati wa Mkutano wa wadau wa Elimu kujenga uelewa wa pamoja kuhusu Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP)uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa elimu walioshiriki Mkutano wa kujenga uelewa wacpamoja kuhusu Mradi wa Kuinua Ubora wa Elimu uliofanyika jijini Dar es Salaam
………………………………………………………………………
◼️Wadau wa Elimu waahidi kushirikiana na Serikali utekelezaji wa SEQUIP
Serikali inatekeleza Mradi wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 500 ambao una lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili wanafunzi katika kupata elimu.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Elimu Kujenga Uelewa wa pamoja kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema katika kuondoa changamoto mradi huo utajenga miundombinu mipya pamoja na kutoa mafunzo kazini kwa walimu.
Katibu Mkuu Akwilapo amesema Mradi huo pamoja na mambo mengine utajenga shule mpya 1,000 za Sekondari katika Halmashauri mbalimbali nchi nzima zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kila moja pamoja na kujenga shule maalum 26 za kisasa katika ngazi ya Mkoa ambazo zitakuwa mahususi kwa ajili ya wasichana watakaochukua mchepuo wa masomo ya Sayansi.
Ameongeza kuwa kupitia Mradi huo Serikali itafanya upanuzi wa takribani shule kongwe 50 ambazo zitadahili wasichana zaidi ya 100 wa kidato cha tano kwa kila shule ikiwa ni pamoja na kumalizia ujenzi wa maabara zote nchini. Pia utapanua na kuimarisha vituo takribani 50 vitakavyodahili wasichana ambao wameshindwa kumaliza masomo yao katika mfumo ulio rasmi kutokana na sababu mbalimbali.
Sambamba na hilo Mradi huo utajikita katika kutoa mafunzo kazini kwa walimu katika masuala ya kidigitali na ufundishaji wa masomo ya Hisabati na Sayansi ambapo takribani walimu 20,000 watanufaika kwa kupatiwa ujuzi wa ufundishaji utakaoendana na wakati wa sasa.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu amesema Mradi wa SEQUIP utahakikisha kuwa shule ni sehemu salama ya kusoma kwa watoto wa kike na kiume kwa kujenga miundombinu na kuboresha huduma za unasihi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Gerald Mweli amesema Mradi huu ni wa miaka mitano kuanzia 2020/21- 2024/25 na unatarajia kuwafaidisha wanafunzi milioni 6.5 wakiwemo wasichana milioni 3.2.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau wa Elimu walioshiriki katika mkutano huo wameipongeza Serikali kwa kutekeleza Mradi wa SEQUIP na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mradi huu ili kuhakikisha mtoto wa Kitanzania anasoma bila changamoto yoyote.