Home Mchanganyiko Timu ya Simba kuitangaza Makumbusho ya Taifa

Timu ya Simba kuitangaza Makumbusho ya Taifa

0

*******************************

Viongozi wa timu ya Simba ya Dar es Salaam wametembelea makumbusho ya Taifa na kuahidi kuitanganza  kupitia kazi zao ili watu wengi zaidi waweze kutembelea na kujifunza.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Timu hiyo Dkt. Arnold Kashembe amesema kuhamasisha utalii wa nchi ni jukumu la kila mtu, hivyo, ofisi yake iko tayari kufanyakazi hiyo kwa kutumia njia mbalimbali zinazotumika na timu hiyo.

Amesema timu ya Simba inatumia fursa ya Wiki ya Ubingwa kufanya utalii katika vivutio mbalimbali nchini kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania.

“Nchi yetu imebahatika kuwa na vivutio vingi lakini wananchi hawajui hivyo vivutio viko wapi na faida yake kwa nchi yetu” anasema Dkt. Kashembe.

Dkt Kashembe amesema timu ya Simba imeanza kazi hii ya kuhamasisha utalii wa ndani na hivyo, ana imani na wengine watafuata.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbuaho ya Taifa. Dkt. Noel Lwoga aliwapongeza viongozi wa timu ya Simba kwa mafanikio waliyoyapata na maono yao ya kuutangaza utalii wa ndani.

Amesema kuna mambo mengi ambayo yanaweza kufanyika kwa kushirikiana na taasisi yake ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya masuala mbalimbali kuhusu urithi wa asili na utamasuni na kuandaa maonesho ya historia ya Simba ambayo yanaweza kuvuta wadau wengi sana.

Amesema uongozi wa Simba umeonesha njia ambayo inaweza kufuatwa na wengine.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbuaho ya Taifa ametoa hamasa kwa Taasisi nyingine za michezo kama vile Yanga kuiga mfano huu wa watani wao wa jadu Simba, na pia kuomba Taasisi mbalimbali ikiwamo za Serikali zenye kupokea wageni kwa shughuli za mikutano n.k. kuwapeleka kwenye Makumbusho za Taifa za Dar es Salaam, Butiama, Arusha na Songea, na maeneo yake ya malikale kama vile Mji Mkongwe wa Mikindani Mtwara, na Eneo la Hifadhi ya Jiji la Dar es Salaam.