*********************************
Na John Walter-Manyara
Timu ya mchezo wa ngumi mkoa wa Manyara yenye Mabondia 22, inaingia kambini leo agosti 16,2020 tayari kwa kujiandaa na michuano ya kutafuta Klabu bingwa yatakayofanyika Septemba 6 hadi 12, mwaka huu, mjini Babati.
Akizungumza katika mashindano ya ngumi yaliyofanyika kimkoa mjini Babati ukumbi wa The Champions Lounge Mjini Babati usiku wa kuamkia leo, Mwalimu aliepo kambini na timu hiyo, Magoa Haule amesema mabondia hao wameingia kambini ili kujifunza mbinu mbalimbali za kuweza kuwashinda wapinzani wao.
Amesema wawapo kwenye kambi itamsaidia kila mchezaji kujiandaa kimwili na kisaikolojia, pamoja na mbinu mbalimbali za kuwateka wapinzani.
Katibu Tawala mkoa wa Manyara Misaile Musa amewataka wafanyabiashara wa mkoa wa Manyara wajitokeze kuiunga mkono timu hiyo kwa kuidhamini na kuwapatia mahitaji muhimu yatakayowasaidia kipindi chote wawapo kambini hapo.
Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amesema kufanyika kwa mashindano hayo ya kutafuta klabu bingwa taifa katika mkoa wa Manyara, ni fursa kwa mkoa kujitangaza na kuongeza uchumi kutokana na wageni mbalimbali watakaokuja kushuhudia mashindano hayo.
Ameongeza kuwa mashindano hayo yatasaidia pakubwa kutangaza vivutio vilivyopo katika mkoa huo hivyo kuwataka wadau mbalimbali kuiunga mkono timu yao.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga amepongeza kamati ya maandalizi ya mashindano hayo na kuahidi ushirikiano.
Kwa upande wao wachezaji wameahidi kufanya vizuri kuuwakilisha mkoa wa Manyara kwani uwezo wanao kutokana na mafunzo waliyopatiwa na walimu wao.
Mwalimu amesema kambi imeanza leo rasmi kwa ajili ya michuano hiyo na hivyo kuahidi kuwafua vijana ili waweze kufanya vizuri katika mashindano hayo yanayohusisha timu mbalimbali kutoka Tanzania bara na visiwani ndani yake zikiwemo timu za majeshi ya Tanzania.
Afisa Michezo mkoa wa Manyara Charles Maguzu amesema mazoezi yao watakuwa wakifanya kila siku asubuhi kwenye Ukumbi wa Ccm Babati mjini.