Mkurugenzi wa Dijitali na Huduma za Ziada Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam jana kuhusu mchakato wa shindano la kuibua vijana wa kitanzania wenye wazo la ubunifu wa teknolojia (Vodacom Digital Accelerator) ambapo siku ya jumanne watatangaza washindi watatu walioshinda shindano hilo, zaidi ya kampuni chipukizi 500 waliwasilisha mawazo bunifu kutoka kote nchini. Wengine kulia ni Mwendesha Mradi Mwandamizi wa SmartCode, Isaack Shayo na Meneja Mradi huo Sharron Nsule.
**************************************
Tarehe 14 August 2020, Dar es Salaam, Tanzania Kampuni ya simu za mkononi inayoongoza kidijitali nchini, Vodacom Tanzania Plc na Kampuni ya Smartcodes leo wametangaza kufikia kwa fainali za mchakato wa “Vodacom Digital Accelerator,” mpango ambao una lengo la kuwasaidia wabunifu chipukizi katika sekta ya teknolojia kuweza kubuni na kuendesha biashara yenye tija kwa jamii na faida kwao.
Mkurugenzi wa Dijitali na huduma za ziada wa Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc Bwana Nguvu Kamando amesema kwamba ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania na Smart Codes ni mwenendo muhimu sana katika kuelekea kwenye utoaji wa fursa kwa biashara zinazochipukia katika mwelekeo wa teknolojia.
“Ninawapongeza washiriki wote kwa kufika katika hatua hii na ninawatakia kila la kheri wakati tunapoelekea katika fainali za mashindano haya. Mara zote Vodacom inakusudia kuleta mabadiliko yenye athari nzuri katika jamii ambako tunaendesha shughuli zetu kuendana na mkakati wetu wa kibiashara. Kwa hivyo mpango wa Vodacom Accelerator una lengo la kutekeleza azma hiyo na kutoa fursa kwa vijana kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi kupitia katika kutatua changamoto za jamii.
“Tunafuraha sana kusikia vijana chipukizi wakitoa mawazo yao ya kiteknolojia na tunamatumaini kwamba watu wengi watakuwa wanatuangalia kushuhudia kampuni za wavumbuzi wakionyesha jitihada zao katika Afrika. Tunatarajia wananchi wote kushuhudia tukio hili, kwa vile siku hiyo ya jumanne ya tarehe 18 mwezi huu, tukio litaoneshwa mubashara kupitia kurasa zetu za mitandao ya kijamii,” alibainisha Bwana Kamando.
Mwendesha Mradi Mwandamizi wa Smart Codes Bwana Isaac Shayo amesema kwamba ushirikiano na kampuni ya Vodacom Tanzania PLC ni kama kichocheo cha kuleta uvumbuzi nchini, jambo ambalo ni muhimu sana katika kutatua changamoto za watanzania kwa kutumia vipaji na masuluhisho ya ndani.
“Mpango wa Vodacom Digital Accelerator Tanzania umekuwa ni mfano bora kwa mashirika na makampuni kushiriki katika uvumbuzi wa vipaji chipukizi. Ni wito kwa wavumbuzi wote, wajasiriamali, na wanateknolojia kutekeleza jitihada kama hizi ambazo zinaweza kubadilisha jamii ya kitanzania kwa kutengeneza masuluhisho bora, kutatua tatizo la kukosa ajira nchini na kuchangia katika kukua kwa uchumi kwa ujumla.” Alieleza Bwana Shayo.
“Siku ya Jumanne tarehe 18 August 2020 itakuwa ni mwisho wa programu na mwanzo wa safari mpya kwa wajasiriamali bora chipukizi watakaochaguliwa pamoja na wajasiriamali wote wengine walioko katika mpango huu. Tukio hili litakuwa ni jukwaa la wajasiriamali chipikizi wa teknolojia kutoa mawazo yao yenye kuleta mageuzi katika jamii. Tukio hili litatangazwa moja kwa moja katika kurasa zetu za Instagram, Youtube na Facebook na tunasisitiza watu wote kujiunga nasi na kushuhudia tukio hili la kusisimua,” alihitimisha Bwana Isaac.
Kampuni za Vodacom Tanzania na Smart Codes ni miongoni mwa wahamasishaji na wawezeshaji wakubwa wa maendeleo ya teknolojia nchini. Wakitumaini kuendelea kuwa wawezeshaji wa maendeleo ya teknolojia na ushirikiano wenye matokeo chanya miongoni mwa wadau wa uvumbuzi nchini Tanzania.
Kuhusu Vodacom Tanzania
Vodacom Tanzania PLC ni watoa huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi na watoa huduma za kifedha kupita simu za mkononi wanaoongoza. Tunatoa huduma mbalimbali za mawasiliano kwa wateja na makampuni – ikiwemo sauti, data na ujumbe mfupi, video, cloud hosting, masuluhisho ya simu za mkononi na huduma za kifedha – kwa zaidi ya wateja milioni 14.1. Kampuni ya Vodacom Tanzania pamoja na kampuni zake tanzu ni sehemu ya Kundi la makampuni ya Vodacom (Vodacom Group) iliyosajiliwa Afrika Kusini , ambayo kwa upande mwingine inamilikiwa na kundi la makampuni la Vodacom Plc la Uingereza. Kampuni ya Vodacom imesajiliwa katika soko la hisa la Dar es salaam (DSE) kwa namba ISIN: TZ1886102715 Stock name: VODA.
Kwa taarifa zaidi , tafadhali tembelea tovuti: www.vodacom.co.tz
Kuhusu Smart Lab:
Smart Lab ni jukwaa la uvumbuzi ambalo linaunganisha taasisi za kielimu na mashirika kwa dhumuni la kuwezesha utengenezaji wa masuluhisho bora zaidi ambayo yataleta athari katika jamii ya Kiafrika.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali tembelea [email protected]