****************************
NA WAMJW- MANYARA
MKURUGENZI wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa Watoa huduma za Afya nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili wakati wa kumhudumia mgonjwa.
Dkt. Grace Magembe ametoa rai hiyo leo, wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya, na ujenzi wa miundombinu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.
Dkt. Grace amesema kuwa, kwa kiasi kikubwa Serikali imewekeza kwenye ujenzi wa miundombinu, vifaa tiba na hali ya upatikanaji wa dawa, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya utoaji huduma za afya bora kwa mwananchi katika jamii.
“Serikali imewekeza kwenye miundombinu, kwenye vifaa tiba, hali ya upatikanaji wa dawa, lakini Watumishi wanatakiwa wafanye kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao wakati wa kumuhudumia mgonjwa ” alisema Dkt. Grace.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali imekuwa ikisisitiza sana, kuhusu maadili mazuri wakati wa utoaji huduma kwa wateja, pindi wanapokuja kupata huduma, hii inajumuhisha mapokezi yake, muda anaotumia kusubiri huduma, muda wa kurejesha majibu yake na kauli zinazotumika wakati wa utoaji huduma.
Hata hivyo, Dkt. Grace ametoa wito kwa viongozi wa hospitali kuwa na mpango madhubuti wa matengenezo ya vifaa tiba ili kuepuka ewezekano wa kusimama kwa baadhi ya huduma, hali itayopelekea wananchi kukosa huduma na upotevu wa mapato.
“Kitu kingine ambacho tunasisitiza katika hospitali ni kuwa na mpango madhubuti wa matengenezo ya vifaa tiba, vifaa ambavyo vimenunuliwa na Serikali ni vya gharama kubwa mnoo, fedha nyingi sana zimetumika, kwahiyo tunasisitiza kuwa na mpango wa matengenezo” alisema
Aidha, Dkt. Grace kwa kiasi kikubwa ameridhishwa na hali ya upatikanaji wa dawa katika maeneo alipofanya ziara, huku akitoa rai kwa Watoa huduma kuhakikisha mgonjwa anapoandikiwa dawa azipate dawa alizoandikiwa lakini pia azipate kwa kwa muda sahihi.
” tumeangalia tena suala la upatikanaji wa dawa, namna dawa inavyohifadhiwa, namna dawa inavyotumika, namna dawa inavyotoka chumba cha kuhifadhia mpaka inapomkuta mhitaji wodini, hii yote tumeifanyia kazi kwasababu tunataka hizo dawa zitumike kulingana na mahitaji yaliyotakiwa” alisema Dkt Grace.
Mbali na hayo, Dkt. Grace amesisitiza agizo la Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi juu ya kufanya kazi kwa juhudi na ushirikiano ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, huku akisisitiza kuwa, kuweka mikakati thabiti katika mapambano dhidi ya vita hii, na kuweka wazi kuwa vifo vya mama na mtoto vitakuwa ni kigezo cha kuangalia uwajibikaji na utendaji kazi wa Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Waganga wafawidhi.
“Hatutaki kuona mama wa Kitanzania anakufa wakati analeta kiumbe Duniani, vifo vingi vinasababishwa na sababu ambazo zinaweza kuzuilika, lazima kila Mtumishi afanye kazi, kuanzia Mganga Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Wilaya, hospitali zote zilizopo ndani ya Mkoa wake, wote wafanye kazi kwa kushirikiana, wake na mkakati, sisi kama Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI tutaendelea kufuatilia tuone kama vifo vinapungua au la na hatua zitachukuliwa ” alisema.
Nae, Mkurugenzi wa uhakiki ubora huduma Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Eliakim Eliud amesisitiza kuwa, kuongeza kazi za utoaji huduma kwa kuzingatia ubora wa huduma na kufuata miongozo ya kujikinga wakati wa kuwahudumia wagonjwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Damas Kayera ameweka wazi kuwa, Mkoa wa Manyara umeendelea kuwa ma rekodi nzuri juu ya hali ya upatikanaji wa dawa muhimu wa kufikia wastani wa 91%, jambo lililosaidia kupunguza malalamiko kwa wananchi wanaokuja kupata huduma.
“Mkoa unaendelea kuwa na rekodi nzuri ya ongezeko la dawa muhimu, zinazofuatiliwa na Wizara ya afya kwa kila kituo, ambapo kwa kipindi cha nusu mwaka 2020 kumekuwa na wastani wa 91%” amesema.