Home Mchanganyiko WAZIRI KALEMANI AAGIZA MKANDARASI KUKATWA BILIONI 4.76 KWA KUCHELEWESHA KUKAMILISHA MRADI WA...

WAZIRI KALEMANI AAGIZA MKANDARASI KUKATWA BILIONI 4.76 KWA KUCHELEWESHA KUKAMILISHA MRADI WA UMEME

0

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akiwasili katika wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya usambazaji umeme katika vijijini vya Farkwa na Banguma.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa Meneja wa Mkoa wa Dodoma,Frank Chambua alipokuwa akitembelea na kukagua miradi mbalimbali  ya usambazaji umeme katika vijijini vya Farkwa na Banguma.

Mafundi wakiendelea kutandaza nyaya za umeme katika vijiji vya Farkwa na Banguma vilivyopo wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza wakati wa kukagua miradi mbalimbali  ya usambazaji umeme katika vijijini vya Farkwa na Banguma.

………………………………………………………………………………

Na.Alex Sonna, Chemba
Serikali imeelekeza kumkata mkandarasi wa Kampuni ya A2Z INFRA ENGINEERING LIMITED asilimia Kumi ya mshahara sawa na shilingi bilioni 4 .76 kwa kuchelewesha kukamilisha mradi wa usambazaji wa umeme katika baadhi ya vijijii vya wilaya ya  Chemba Mkoani Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya usambazaji umeme katika vijijini vya Farkwa na Banguma wilayani humo.
Aidha Dkt. Kalemani ametoa maamzi hayo baada ya kuona kuwa mkandarasi huyo alitakiwa kukamilisha mradi huo tarehe Juni 30 mwaka huu.
“Hatuongezi fedha na miradi hii ikamilike kwa wakati kwani mko nje ya muda huku wananchi wanahitaji huduma ya umeme na mkiwalipa mtakatwa mishahara yenu”,amesisitiza Dkt. Kalemani.

Hata hivyo Dk.Kalemani amemtaka  Mkandarasi huyo kukamilisha kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji vyote 66 vilivyobakia kabla ya Septemba 15 mwaka huu, huku akisisitiza kuwa, hakutakuwa na nyongeza ya muda wala msamaha.

Kwa kuongezea Dkt. Kalemani amewataka wakandarasi wote nchini wanaotekeleza Mradi wa REA kuwa wamekamilisha usambazaji wa umeme ifikapo Sept 15 mwaka huu.
“Maeneo yatakayokuwa yamebaki fanyeni nyinyi TANESCO kukamilisha miradi hiyo ya usambazaji umeme na pesa iliyokuwa ilipwe kwa hao wakandarasi ilipwe kwenu”, ameelekeza Dkt. Kalemani.
Pia Dkt. Kalemani ametoa siku 10 kufungwa transifoma katika kijiji cha Mtoro ,Gonga,Babahi na Makorongo na siku ya tarehe 22 Augusti mwaka huu anakwenda kuwawashia wananchi wa vijiji hivyo umeme.

Katika kuhakikisha kazi hiyo inatekelezwa, Waziri alimwelekeza Mkuu wa Wilaya kushikilia hati za kusafiria za Wakandarasi husika na kuhakikisha hawatoki nje ya Mkoa wa Dodoma, hadi watakapokamilisha kazi hiyo.

Aidha, alimwagiza Mkandarasi huyo kuongeza vibarua na magenge, ili aweze kukamilisha kazi kwa wakati.

Hata hivyo Dkt. Kalemani ameagiza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma kumuweka pembeni msimamizi wa mradi wa REA Mkoa wa Dodoma baada ya kushindwa kusimamia majukumu kikamilifu.
“Hatuwezi kufanya kazi kwa mazoea hivyo mkandarasi atakayeshindwa kukamilisha na kukabidhi mradi wake Septemba 15 mwaka huu na watendaji wote wa REA watachukuliwa hatua za kisheria kwani wananchi wanahitaji kupata huduma ya nishati ya umeme nyinyi mnaleta mazoea kazini”, amesisitiza Dkt. Kalemani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amekiri kuwepo utendaji mbovu wa mkandarasi huyo kwa kuwemo kutoonekana  kazini kwa kipindi cha miezi sita.
“Mhe. Waziri nakuhakikishia kuwa maelekezo yote uliyonipa nitayatekeleza kikamilifu na kwa wakati na kuhakikisha wananchi wetu wanapatiwa huduma stahiki”, amesema Odunga
Lakini pia Odunga ametoa rai kwa watendaji wa wizara ya nishati kuwa inapotokea miradi mingine ya usambazaji wa umeme vijijini wale wakandarasi waliyoshindwa kutekeleza miradi yao kwa wakati wasipewe mikataba tena kutokana na kutokuwa wawajibikaji katika miradi waliopewa awali.

Awali akitoa taarifa  yake kwa Waziri, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Frank Chambua alieleza kuwa, kati ya vijiji 581 vya Mkoa huo, vijiji 393 vimeshapata umeme ambavyo ni sawa na asilimia 67.47 ya vijiji vyote.