*****************************
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo amesema hatua ya Serikali ya awamu ya tano kuanzisha Tume ya kupambana na Madawa ya kulevya na kuwezesha Kliniki ya tiba ya waraibu Wilayani Bagamoyo inakwenda kuwa muarubaini wa vita dhidi ya mapambano hayo .
Ameeleza ,waingizaji wa madawa hayo hawana nafasi kwa kipindi hiki na amewataka wananchi wazidi kutoa ushirikiano katika kutokomeza biashara hii kwa kuwataja majina ya wahusika wote ili vyombo vya Dola viwashughulikie.
Hayo aliyaeleza wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendelo na kusikiliza kero za wananchi Wilayani Bagamoyo, ambapo alitembelea na kukagua ukarabati wa jengo la kliniki hiyo iliyopo hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.
Akizungumza na Waraibu mjini Bagamoyo ,Ndikilo alieleza Serikali imefanya jambo jema kwa kuanzisha Kliniki hii ambayo kwa kiasi kikubwa imeweza kuwasaidia Vijana ambao walijiingiza katika matumizi ya madawa hayo.
Aidha alipongeza kwa mpango wa kuanzisha kliniki nyingine ya waraibu katika Hospitali ya Mkoa ya Tumbi.
Ndikilo alisema , waraibu hao kuachana na madawa ya kulevya “Madawa ya kulevya sasa basi, Madawa ya kulevya ni hatari, yanaangamiza utu wa binadamu, yanaua nguvu kazi ya nchi Hongereni kwa uamuzi mliochukua kuachana na madawa hayo” alisema Ndikilo.
Alisema kwamba ,Rais Dkt. John Magufuli tangu aingie madarakani ameendelea kupambana na madawa ya kulevya na kuunda Tume ya kudhibiti madawa ya kulevya Nchini.
“Juhudi zetu zimefanikiwa kupambana na madawa haya, nipongeze jeshi la polisi kwa kupambana na hili, lakini bado ongezeni nguvu na taarifa nazopata za kuripoti uwepo madawa ya kulevya Mkoani Pwani zimepungua”alifafanua Ndikilo.
Mkuu wa Mkoa huyo aliwashauri waraibu hao ,kutengeneza vikundi vya ujasiriliamali ambavyo vitaweza kuwasaidia katika kuinua uchumi wao na kujishughulisha kiuchumi .