Msajili wa Maabara binafsi za Afya Bw. Dominic Fwiling’afu akitoa elimu kwa mtaalamu wa maabara wakati wa ukaguzi wa maabara jijini Dar es Salaam
*****************************************
Na.WAMJW-Dar es Salaam
Wamiliki wa Maabara Binafsi za Afya wameelekezwa kufuata sheria na taratibu zinazosimamia uendeshwaji wa Maabara hizo ili wagonjwa wapate majibu sahihi yatakayopelekea huduma bora za matibabu kwa wagonjwa.
Hayo yamebainishwa na Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi za Afya nchini Bw. Dominic Fwiling’afu wakati wa ukaguzi wa Maabara Binafsi za Afya katika Wilaya zote za jiji la Dar es Salaam.
Bw. Fwiling’afu amesema ukaguzi huo umefanyika kwa lengo la kuangalia hali ya utoaji wa huduma za Maabara Mkoani Dar es Salaam lengo ikiwa ni kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za Maabara ambazo zitawasaidia matabibu kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
“Katika ukaguzi wetu tumepita katika Wilaya zote za jiji la Dar es Salaam, tumefanya ukaguzi, tumetoa elimu , ushauri na maelekezo magine ili kuboresha huduma. Lakini pia kuna baadhi ya Maabara tumelazimika kuzifungia kwani zimekua zikiendeshwa kwa kukiuka sheria Na. 10 ya Mwaka 1997 Pamoja na kuhatarisha maisha ya watanzania wanaofika kupata huduma katika vituo hivyo” Alisema Bw. Fwiling’afu
Amesema Pamoja na kuzifungia baadhi ya Maabara ambazo zimekua zikiendeshwa kwa kukiuka sheria zipo Maabara ambazo zimepongezwa kwa kutoa huduma bora kwa kufuata sheria na miongozo na hivyo kupelekea wananchi kupata huduma bora za Maabara.
Kwa upande wake Mratibu wa huduma za Maabara Wilaya ya Ilala Petrobas Hassan ameishukuru Wizara ya Afya kwa kufanya ukaguzi huo katika jiji la Dar es Salaam kwa kuwa kuna maabara nyingi na zinahitaji kujengewa uwezo ili zitoe huduma bora kwa wananchi.
“Naishukuru sana Wizara ya Afya kupitia Bodi ya Maabara Binafsi za Afya, kwa kuja kufanya ukaguzi huu, mimi kama maratibu nimefarijika sana maana ninaowasimamia wamepata elimu, ushauri Pamoja na maelekezo mengine yanayolenga kuboresha huduma hivyo nashauri ukaguzi huu ufanyike mara kwa mara ili kuendelea kuboresha huduma” Alisema Bw. Petrobas
Mtaalam wa maabara kutoka kituo cha Ibrahim Haji cha jijini Dar es Salaam Bw Deogratious ameishukuru Wizara ya Afya kwa kufanya ukaguzi na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Maabara jambo ambalo limewaongezea ujuzi na maarifa katika kufanya kazi zao za kila siku na kuhakikisha wananchi wanapata majibu sahihi kwa wakati ili kupata tiba bora.