……………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKUU wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo amesema ,Mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (Standard Guage Railway-SGR) ni mradi wa kielelezo katika Taifa na kwamba baadhi ya wananchi wa Mkoa huo ,wanaendelea kunufaika nao hasa upande wa ajira .
Aidha ,kuhusu fidia kwa ajili ya Taasisi na Wananchi waliopisha upanuzi wa Reli hiyo na kutoa maeneo yao kwa ajili uchimbaji vifusi, Ndikilo amesema fedha zimeshapatikana na wahusika wote wataanza kulipwa.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo eneo la Ruvu stesheni wilayani Kibaha,alisema mradi huo mkubwa wa kimkakati umeshatoa ajira 300 za moja kwa moja kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani, huku makampuni makubwa Mkoani hapo yamefaidika kwa kutoa huduma na bidhaa ambazo ni Nondo, Kokoto na Chakula.
Aidha,Ndikilo alisema Serikali kupitia mradi huo imejenga kituo cha kuhifadhia Mboga mboga eneo la Ruvu stesheni( Freight station) hivyo uwepo wa kituo hiki utaamsha ari ya kilimo cha mboga mboga katika bonde la Mto Ruvu na kukuza biashara hiyo.
Hata hivyo Ndikilo alieleza , Mkoa unaendelea kusimamia ulinzi na usalama wa mradi huo na kwamba hakuna wizi mkubwa wa vifaa vya ujenzi.
“SGR inakwenda kuwa mkombozi katika kurahisisha usafirishaji wa mizigo na watanzania hivyo usafiri kuwa rahisi na uhakika kupitia njia ya reli ya kisasa”:; anasema mkuu huyo wa mkoa .
Katika hatua nyingine,maendeleo ya ujenzi unaendelea katika kipande cha kwanza na cha pili katika awamu ya kwanza ya ujenzi Dar es salaam -Mwanza.
Katika kipande cha kwanza Dar es salaam-Morogoro ujenzi umefikia asilimia 87 huku Morogoro-Makutupora ujenzi wa reli umefikia asilimia 36.8.5.