……………………………………………………………………………..
Na. Catherine Sungura-WAMJW-Dodoma
Wauguzi nchini wametakiwa kujiendeleza ikiwemo kujifunza vitu vipya ili kuweza kwenda na wakati katika kuongeza viwango vyao vya utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe wakati akifunga kikao kazi cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi Wauguzi Wakuu wa Wilaya wapatao 89 kutoka wilaya 89 nchini.
Prof. Mchembe alisema kuwa hivi sasa nchi imeingia kwenye uchumi wa kati hivyo kwenye sekta ya afya inapaswa kuboresha huduma zenyewe ,vifaa na vifaa tiba pamoja na kuwa na stadi za kutosha kwa watumishi ili huduma zitolewazo ziwe na ubora wake.
“Mnapokua pamoja mnachangiana na kusaidiana mawazo ili muweze kuboresha huduma kwenye vituo vyenu lakini mtakaporudi ni vyema mkawahusisha wenzenu kwani kila mmoja ana mawazo yake na yakichukuliwa yataeleweka,sio ukiwa Muuguzi Mkuu wa wilaya au mkoa basi unajua kila kitu ni vyema mkayaheshimu mawazo ya wengine”Alisisitiza.
Aidha, Prof. Mchembe amesema kuwa wauguzi waliopo halmashauri na hospitali za rufaa wote ni sawa na wanafanya kazi za aina moja hivyo wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili kwa kutenda kufuatana na taaluma yao.“Kutofufanya kinyume na fani yako ni muelekeo mzuri hivyo kukutana hapa mmeweza kukumbushana maadili yenu kwahiyo mnapaswa mkaendeleze mliyojifunza hapa mtakaporudi mkawafundishe wenzenu kwenye sehemu zenu za kazi”.
Akijibu azimio la upande wa mafunzo Katibu Mkuu huyo alisema amekubaliana na uwepo wa utaratibu wa kufuatilia vyuo vya mafunzo kwa idara ya mafunzo inapaswa kuwa na dawati la uwakilishi ili watakaochaguliwa wawe wanawakilisha kulingana na mahitaji na kushirikiana na wauguzi ili kuona ni upande gani wanapaswa kupatiwa mafunzo yapi kulingana na muundo pia.
Hatahivyo amewataka wanapomaliza vikao wawe wameweka vipaumbele na muda wa tekelezaji ili kurugenzi ya uuguzi na ukunga waweze kuifanyia kazi ikiwemo changamoto wanazokabiliana nazo sehemu zao za kazi.
Kikao kazi cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi wauguzi wakuu wa wilaya kimefanyika kwa siku tatu jijini hapa kwenye ukumbi wa Cathedral ambapo imewakutanisha wauguzi wakuu wa wilaya 89 kutoka mikoa kumi na mbili ambapo yaliandaliwa na Baraza wa Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC).