Wawakilishi wa vyama vya siasa wilayani Busega kwa makini wakisikiliza maelekezo ya maadili kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 2020.
*********************************
Vyama vya siasa wilayani Busega vyatakiwa kufuata maadili, taratibu na kanuni za uchaguzi Mkuu wa kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Anderson Njiginya Kabuko wakati wa kikao na Viongozi wa Vyama vya Siasa wilayani Busega kilichofanyika tarehe 05/08/2020.
Ndugu Kabuko ambaye ni Msamizi wa Uchaguzi Jimbo la Busega, amevitaka vyama vya siasa vilivyopo wilayani Busega kuwa na utulivu na kufuata sheria na kanuni za uchaguzi kuelekea uchaguzi mkuu na kuwaasa kuteua wagombea watakaokuwa na mawazo chanya hivyo kukubalika na wananchi.
Utakapofika muda sahihi wa kufanya kampeni, tufanye vizuri kampeni kwa kuzuia taharuki, kuzuia mihemko na uchochezi ili kupita salama katika jambo hilo, na naomba Mwenyezi Mungu atusimamie tuweze kusimamia salama mpaka mwisho wa zoezi hili, aliongeza Ndugu Kabuko.
Kwa upande mwingine Kabuko amevitaka vyama vya siasa na wagombea wao kujikita hasa katika sera na sio vingenevyo, hii itasaidia kuwa na hoja ambazo hazitakuwa na uchochezi hivyo kuzuia vurugu na taharuki kwa wapiga kura.
Awali mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Ndugu Rutagumirwa Rutalemwa amesisitiza vyama vya siasa na wagombea watakaopata nafasi ya kugombea kuzingatia maagizo ya maadili yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi ili nchi yetu iweze kupita salama kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba. Ameongeza kwamba vyombo vya usalama na ulinzi wilyani Busega vitafanya kazi kwa muda wote ili kuhakikisha amani inatawala kwa kipindi chote cha uchaguzi. Tutumie lugha za ustarabu na staha ili kuepuka lugha za matusi na tuheshimu utu wa mtu, alisema Ndugu Rutalemwa.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Busega Bw. Hamad Mabula amewaomba wawakilishi hao wa vyama vya siasa kwamba TAKUKURU itakua macho muda wote na haitasita kuchukua hatua kwa mtu yoyote kutoka chama chochote atakayefanya vitendo vitakavyoashiria rushwa. Tutamkamata, kumhoji na kumfikisha mahakamani mtu yoyote wakati na baada ya uchaguzi kama tutakuwa na mashaka ya vitendo vyovyote vya kuashiria rushwa, aliongeza Bw. Mabula.
Jumla ya vyama vitano (5) vya siasa vilivyothibisha ushiriki wao katika uchaguzi mkuu wilayani Busega, vimeweza kushiriki katika kikao hicho ambacho kilimalizika kwa wawakilishi hao kufurahishwa na hatua mbalimbali zinazoendelea kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu. Vyama vilivyoshiriki ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Civic United Front (CUF), Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) na United Democratic Party (UDP).
Washiriki wote kutoka vyama vitano vya siasa wametolewa hofu juu ya kutokuwepo na misongamano kwa wapiga kura kwenye vituo ili kutoa fursa kwa kila mwenye sifa ya kupiga kura kutimiza haki ya kikatiba kwa kuchagua viongozi anaowataka, alisema hayo Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Busega Bi. Grace Ishengoma wakati akijibu swali la mwakilishi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Mkeshi Mhoja aliyekuwa na hoja kuhusu idadi ya wapiga kura kwa kila kituo. Kikao hicho pia kilihudhuliwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo na baadhi ya Watumishi wengine kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega.