Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi akiwa katika Studio za Nyemo FM Redio Jijini Dodoma jana jioni, kuzungumzia Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa Miaka Mitano katika Kipindi Maalum, ambapo alikuwa na Mtangazaji wa kipindi hicho Bw. Bilson Vedastus (hayupo pichani).
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi (Kushoto) akiwa katika Studio za Nyemo FM Redio Dodoma jana jioni, kuzungumzia Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa Miaka Mitano katika Kipindi Maalum, ambapo alikuwa na mtangazaji wa kipindi hicho Bw. Bilson Vedastus Bilson Vedastus (kulia).
…………………………………………………………………..
Na Anitha Jonas – WHUSM,
Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi aeleza adhima ya serikali kuanzisha Kampasi ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya katika Mkoa wa Dodoma na Dar es Salaam kwa lengo la kutoa fursa kwa vijana wengi kujifunza maswala ya michezo.
Dkt.Abbasi ameeleza hayo jana jioni alipokuwa akifanya mahojiano katika Kipindi Maalum kilichokuwa kikirushwa na Nyemo Fm Redio Dodoma, kikizungumzia Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano, ambapo alisema tayari uongozi wa Bodi ya Chuo hicho umekwisha pitisha azimio hilo la kuanzishwa kwa kampasi hizo mbili.
“Serikali imeendelea kuimarisha Miundombinu ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Mwanza, fedha za maendeleo zimekuwa zikitolewa kuimarisha miundombinu na kwa mwaka wa fedha ulionza Julai 2020 chuo kimetengewa fedha kwa ajili ya kuongeza Hosteli, Madarasa, na viwanja vya mazoezi kwa wanafunzi,”alisema Dkt.Abbasi.
Akiendelea kuzungumza katika kipindi hicho cha mahojiano Dkt. Abbasi alieleza kuwa serikali imeweka mifumo ambayo inasimamia sekta ya michezo vyema ikiwemo Bazara la Michezo Taifa (BMT) kwa kushirikiana na mashirikisho mbalimbali, na katika serikali ya awamu ya tano sekta hiyo imefanikiwa kuongeza hamasa kwa wananchi kushiriki michezo kwa lengo la kuimarisha afya zao.
Vilevile alieleza kuwa Serikali ya Awamo ya Tano imeendelea kuboresha miundombinu ya Uwanja wa Taifa kwa sasa Uwanja wa Benjamini Mkapa kama Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli alivyotangaza hivi karibuni kubadilisha jina la uwanja huo kwa lengo la kuenzi mchango wa Rais huyo wa Serikali ya Awamu Tatu katika sekta ya michezo pamoja na uwanja wa Uhuru.
Pamoja na hayo kwa upande wa Sekta ya Habari Dkt.Abbasi alifafanua kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 na hoja zinazoibuka kuhusu kubanwa kwa uhuru wa vyombo vya habari kwa kusisitiza hakuna uhuru usiyo na mipaka kwani hata mataifa makubwa ya nje nayo yana mwongozo katika usimamizi wa masuala ya habari.
Halikadhalika Katibu Mkuu huyo na Msemaji Mkuu wa Serikali alifafanua kuwa habari ni taaluma na kila taaluma inamisingi na miiko ya taalamu yake na baadhi ya wanahabari wanachanganya dhana ya uhuru na miiko ya taaluma,kwa kusema kwanza ujio wa sheria hii ni jambo la kujivunia kwa wanahabari, pia ni mafanikio ya serikali ya awamu ya tano, sababu kwa miaka mingi hakukuwa na sheria habari bali kulikuwa na Sheria ya Magazeti.
Aidha, Dkt. Abbasi alifafanua kuwa sheria hiyo ya habari imeweka mawanda mapana ya kusimamia ukuaji wa sekta habari kwani imezungumzia haki za wanahabari, uanzishwaji wa taasisi mbalimbali za kusimamia taaluma ya habari, pamoja na kutoa mwongozo wa kuzingatia miiko ya taaluma kama kuzuia utoaji wa taarifa za uongo, Kuzuia kuchapisha habari za kashfa, pamoja na kushawishi watu kufanya makosa.
Pia alieleza kuwa hivi karibuni wizara hiyo kwa kushirikiana na TCRA wameidhinisha uanzishwaji wa redio 10 ambazo zitakuwa zikifanya kazi, hivyo hakuna kubanwa kwa uhuru wa habari bali ni usimamizi wa miiko na misingi ya taaluma ndiyo serikali ya awamu ya tano inachokifanya.
Halikadhalika nae Dkt.Abbasi alifafanua kuhusu suala la nchi kuingia katika Uchumi wa Kati kwa kueleza mchakato wa kufikia uchumi wa kati ulianza tangu serikali ya Awamu ya Kwanza na Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza jitihada ya kuleta maendeleo kwa kasi na hii ndiyo imesaidia taifa kufikia hatua hiyo.
*******************MWISHO**************